JPM aombwa kutegua utata wa Kiwanda cha NMC Arusha
*Wakulima wailalamikia Bodi ya Nafaka kutumia ‘ubabe’ kukifunga
*Mwekezaji Mzalendo adaiwa ‘kulizwa’ uwekezaji wa Sh, bilioni 13
*Kauli yake inasubiriwa kama Turufu ya ushindi CCM au CHADEMA
NA MWANDISHI WETU, ARUSHA
WAKULIMA wa mazao mchanganyoko katika mikoani ya Manyara na Arusha wamempigia magoti Rais Dkt John Pombe Magufuli, ambaye pia ni Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM kutengua sintofahamu iliyochukuliwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, kukifunga kiwanda cha Unga NMC mkoani humo.
Kiwanda hicho ambacho awali kilikuwa sehemu ya mali za lililokuwa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), lilibinafsishwa mwaka 2007 chini ya Shirika la Hodhi ya Mali za Serikali CHC, kwa kampuni ya kizalendo ya MONABAN Trading andFarming Limited.
Hatua hiyo ya CHC ililenga kukifufua kiwanda hicho kwa nia ya kuwasaidia wakulima wa mazao mchanganyiko kama mahindi na ngano kwa mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, ambapo uwekezaji huo ulielezwa kuwafikia wakulima wengi.
Hata hivyo imebainika kuwa maamuzi ya Bodi hiyo, yameathiri ajira zaidi ya 400 za watu waliokuwa wameajiriwa kiwandani hapo, huku wategemezi wao zaidi ya 4000 wakibaki midomo wazi, kutoelezwa hatma ya jambo hilo, kwa miaka miwili sasa, huku jamii ikitaka kuitumia nafasi hiyo kuiadhibu CCM katika Jimbo la Arusha.
Aidha, uamuzi huo wa Bodi umeendelea kulalamikiwa na wakulima wa mazao hayo kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, ambao wamemuomba Rais Magufuli, anayeendelea na kampeni zake, kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuchukua hatua za haraka kulitafutia ufumbuzi jambo hilo.
Wananchi hao wamedai kwamba kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji za kiwanda hicho, kumechangiwa na mashinikizo ya baadhi ya viongozi waandamizi serikalini, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, ambaye sasa ni Mgombea Ubunge kupitia CCM akikabiliana vibali na Godbles Lema wa CHADEMA.
Wakulima hao wamedai kuwa hatua ya kuitumia Bodi kukifunga kiwanda hicho mapema mwezi Juni mwaka 2018, mbali na kuwaathiri wananchi wengi kiuchumi, ilikuwa na nia ya kumdhibiti mmiliki wa kampuni ya Monaban Trading and Farming Limited, ambaye ni kada wa CCM mwenye nguvu kugombea Ubunge katika Jimbo hilo la Arusha.
“Tumefikia hatua ya kumuomba Rais, kuchukua hatua za haraka kulitafutia ufumbuzi jambo hili, siasa zisichangie umasikini, tumefunga kiwanda, hakuna kitu kinachoendelea, ajira zaidi ya 400 zimepotea, lakini pia wakulima wamepoteza soko la uhakika la mazao yao,” alisema Mwenyekiti wa Mazao ya nafaka katika mikoa ya Arusha , Kilimanjaro na Manyara Matrida Koisela.
Mama Koisela, mkazi wa Ngarenalo Jijini Arusha, alisema vijana 400 waliopoteza kazi kwenye kiwanda hicho ni wakazi wa Arusha mjini, lakini pia wategemezi wao pia ni wakazi wa Arusha, hivyo kukosekana kwa utayari kiuhusu jambo hilo, kunaweza kuwa turufu kwa CHADEMA.
“Vijana wana hasira, mitaani wanasema hadharani, Gambo ameshiriki kufungwa kwa kiwanda ambacho wao walikuwa wakipata mkate wao wa kila siku, leo CCM imemleta Gambo kugombea katika jimbo hilo,” alisema.
Wakulima hao walisema kuwa, “Kwa sasa kauli Rais Magufuli, ndio inayosubiriwa na wengi na hasa wananchi wa Jiji la Arusha, kuhusu uhalali wa kufungwa kwa kiwanda hicho, ama kufunguliwa na kurejesha imani kwa watu wengi walioumizwa na jambo hilo,” walisema wakulima hao
Kwa mujibu wa wananchi hao, Mwekezaji Mzalendo huyo aliyenyang’anywa uendeshaji wa kiwanda hicho, alijitahidi kuwekeza zaidi ya Bilioni 13 kufufua kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kazi ya kufufua kivu cha kukoboa na kusaga unga wa ngano na mitambo mingine.
“Huu ni uwekezaji mkubwa, tena umefanywa na mtanzania mzalendo, jambo hli halipaswi, kuachwa likapita hivi hivi, lakini imani yetu, muhusika mkubwa na mwenye maamuzi ya mwisho ni Rais Magufuli,” walisema.
Jitihada za kumtafuta Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, kuzungumzia jambo hilo zilishindikana, kutokana na kutopatikana kwa simu yake ya kiganjani, lakini pia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Monica Mbega, hakuwa tayari kulizungumza suala hilo.
Taarifa za baadaye zilizopatikana, zilisema kuwa Bodi hiyo ilikuwa ikitaka kuingia ubia wa kuendesha kiwanda hicho na mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Asia, ambaye jina lake kwa sasa linahifadhiwa, anayedaiwa pia kuwa mshirika wa karibu wa mwanasiasa mmoja mkoani Arusha.
No comments: