AL AHLY SC YATANGULIZA MGUU MMOJA FAINALI YA LIGI MABINGWA AFRIKA (CAF CL)

Na Bakari Madjeshi,  Michuzi TV

Klabu ya Soka ya Al Ahly ya nchini Misri imeanza kuonyesha nia ya kutwaa taji la Tisa la Michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika baada ya kuitandika Wydad Athletic Club ya Morocco bao 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Michuano hiyo uliopigwa kwenye dimba la Mohammed V nchini Morocco.

Mchezo huo uliokuwa wa kuvutia dakika zote 90,  Al Ahly waliokuwa chini ya Kocha wao mpya,  Pitso Mosimane walionyesha matumaini ya kufika Fainali ya Michuano ya CAF kwa ngazi ya vilabu kwa kutandaza kabumbu safi ugenini nchini Morocco.

Dakaki za mwanzo tu,  Al Ahly walionyesha matumaini hayo baada ya kupata bao safi dakika ya 4 ya mchezo kupitia kwa Kiungo wake,  Mohammed Magdy ambaye alitumia makosa ya mabeki wa Wydad Casablanca waliokuwa katika harakati za kuondoa hatari langoni mwao.

Wydad Casablanca wakiwa nyumbani walipata penati dakika ya 42 ya mchezo ambayo ingeweza kusawazisha bao hilo lakini kwa bahati mbaya, Penalti hiyo iliyopigwa na Mchezaji,  Yahya Jabrane iliondolewa na Golikipa wa Al Ahly, Mohammed El Shenawy. 

Dakika ya 62 ya mchezo, Al Ahly walipachika bao la pili kupitia kwa Ali Maáloul kwa mkwaju wa Penalti baada ya Beki wa Wydad kushika mpira uliopigwa na Nyota wa Al Ahly, Junior Ajayi katika eneo la hatari. 

Matokeo hayo yatasubiri mchezo wa marudiano utakaopigwa Oktoba 23,  2020 mjini Cairo nchini Misri,  mchezo ambao utaamua mshindi ambaye atacheza Fainali ya Michuano hiyo kati ya Zamalek au Raja Casablanca.



 

No comments: