WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YAKANUSHA KUSHIRIKIANA NA SHIRIKA LA BCC KUTOA MITAJI YA KILIMO BILA RIBA



Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, akitoa taarifa kwa umma akikanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Wizara ya Fedha na Mipango inashirikiana na Shirika binafsi la BACC kutoa mitaji ya biashara na kilimo bila riba wala vikwazo, ofisini kwake jijini Dodoma. Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma. (Picha na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma)

***********************************

Na. Peter Haule na Ivona Tumsime, WFM, Dodoma

Wizara ya Fedha na Mipango imekanusha taarifa inayosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa inashirikiana na Shirika binafsi la BACC kutoa mitaji ya biashara na kilimo bila riba wala vikwazo.

Akiongea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja, amesema taarifa hiyo ipuuzwe kwa kuwa Wizara inautaratibu maalumu wa kufikisha taarifa kwa Umma

“Wizara hutumia njia rasmi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliyosajiliwa na kutambulika na Serikali kutoa taarifa zake, hivyo ni vema kutambua kuwa Wizara haihusiki katika taarifa hizo zenye lengo la kupotosha umma na kuibua sintofahamu miongoni mwa jamii”, alisema Bw. Mwaipaja.

Ameitaka jamii kujihadhali na genge hilo la matapeli wanaotumia mitandao ya kijamii kuwarubuni ili kujipatia fedha za wizi.

Alisema kuwa Wizara haitambui na wala haijawahi kujihusisha kwa namna yoyote na kampuni hiyo na wala Wizara haina mradi wowote wa namna hiyo wa kuwakopesha wafanyabiashara na wakulima mikopo isiyo na riba wala vikwazo.

“Hao ni matapeli wa kimtandao, wapuuzeni”, alisisitiza Bw. Mwaipaja

Aidha, amewaonya watu wanaofanya vitendo hivyo kuacha maramoja kwani wanatafutwa na vyombo vya dola kwa udi na uvumba na kwamba wakipatikana hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Bw. Mwaipaja amewataka wote ambao watapenda kupata maelezo ya ziada kuwasiliana na Kitengo cha Mawasilaiano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Namba ya simu ya mkononi 075481562.

No comments: