TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUZINGATIA KIKAMILIFU SHERIA YA SERIKALI MTANDAO

 

 

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUZINGATIA KIKAMILIFU SHERIA YA SERIKALI MTANDAO


Charles James, Michuzi TV


TAASISI za Umma zimetakiwa kuzingatia kikamilifu sheria ya serikali mtandao ya mwaka 2019 na kanuni zake za mwaka 2020 katika kutekeleza jitihada za serikali mtandao mahala pa kazi.


Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa kufungua mafunzo kwa wakuu wa idara na vitengo vya Tehama serikalini yenye lengo la uelewa katika kutekeleza sheria ya serikali mtandao na kanuni zake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu Serikali, ACP Ibrahim Mahumi amesema mafunzo hayo yatakua chachu kwa watumishi hao kuelewa sheria hiyo na kanuni zake.


ACP Mahumi amesema serikali kupitia tangazo Na. 964 la Desemba 6, 2019 ilitangaza kuwa Desemba 15 mwaka huo ni siku ya kuanza kutumika rasmi kwa sheria hiyo ya serikali mtandao na kanuni zake zilipitishwa mwanzoni mwa mwaka 2020 ambazo nazo zimeanz kutumika katika kutekeleza sheria hiyo.


Amewataka washiriki hao wa mafunzo kutambua kuwa sheria iyo inaweka misingi ya kisheria wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Tehama ya mwaka 2016 na kuanzisha mamlaka ya serikali mtandao (e-GA) yenye jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendeleza utekelezaji wa Serikali mtandao pamoja na kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali mtandao katika taasisi za umma.


" Nazipongeza taasisi za umma ambazo zimefanikiwa kuboresha utendaji kazi na kutoa huduma zao kwa umma kwa kutumia Tehama, ingawa tunaelewa kumekua na changamoto katika eneo hili kama vile uwepo wa mifumo isiyoongea na urudufu.


Sheria hii itasaidia kutatua baadhi ya changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kuiwezesha mamlaka ya serikali mtandao kutoa viwango na miongozo ya kitaalamu vya serikali mtandao kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa jitihada mbalimbali za serikali mtandao katika taasisi za umma," Amesema ACP Mahumi.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Dk Jabiri Bakari amesema mafunzo haya ya leo yatawapa uelewa kuhusu vifungu mbalimbali vya sheria hiyo na kanuni zake pamoja na mabadiliko yanayotokana na sheria hiyo ikiwemo kuibadili kutoka kuwa Wakala ya Serikali Mtandao kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao pamoja na majukumu ya mamlaka hiyo.


" Niwasihi washiriki wote wa mafunzo kuzingatia kile kitakachotolewa leo lakini pia wakawe watumiaji wazuri wa Sheria hii maana wote tunajua sheria ni msumeno watakaokiuka watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni," Amesema Dk Jabiri.


 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wakuu wa vitengo vya Tehama serikalini yaliyofanyika leo jijini Dodoma.

 Washiriki kutoka Taasisi na Ofisi mbalimbali za serikali ambao wamehudhuria mafunzo ya wakuu wa vitengo vya Tehama serikalini juu ya uelewa katika kutekeleza sheria ya Serikali Mtandao na kanuni zake.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Dk Jabiri Baraka akizungumza na wandishi wa habari baada ya mafunzo kwa wakuu wa vitengo vya Tehama serikalkni kufunguliwa.

No comments: