PROFESA MGAYA AIPONGEZA NIMR MBEYA KWA UMAHIRI WAKE KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UTAFITI

 

Na Chalila Kibuda, Bagamoyo Pwani

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Yunus Mgaya amempongeza Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha NIMR Mbeya Dakta Nyanda Elias Ntinginya kwa umahiri wake katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi ya utafiti ukiwemo utafiti wa HOPE unaolenga katika kuimarisha shughuli za upimaji wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa Watoto wachanga waliozaliwa na akina mama wenye maambukizi ya VVU; hatua ambayo imekiwezesha kituo hicho cha NIMR Mbeya kufikia malengo ya miradi yake kwa wakati na utimilifu.

Profesa Mgaya amesema taarifa ya matokeo ya awali ya utafiti wa HOPE inaashiria kuwa mradi huo utachangia kuimarisha udhibiti wa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au  wakati wa kunyonyesha.

Akizungumza mjini Bagamoyo mkoani Pwani katika Mkutano wa Wadau wa Utafiti  wa HOPE uliolenga kujadili matokeo ya awali ya utafiti wa mradi huo; Profesa Mgaya amesema ushirikishwaji mzuri wa wafanyakazi katika mradi na matumizi sahihi na ya wakati ya fedha; yamechochea kwa kasi utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kutoa matokeo yake rasmi ifikapo mwezi Desemba 2020.

 “NIMR Mbeya iko mstari wa mbele kutumia ubunifu katika utekelezaji kazi za kitafiti na kujengea uwezo watafiti na viongozi wake wakiwemo viongozi wa miradi hatua ambayo inaashiria kuleta matokeo chanya ya kisekta na Taifa kwa ujumla hata katika mradi huu wa HOPE.” Alifafanua Profesa Mgaya.

Utafiti wa HOPE unafanywa na NIMR kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) chini ya ufadhili wa Global Fund na ulianza kutekelezwa rasmi mwezi April 2020. Utafiti huu unatekelezwa katika mikoa 18 ya Tanzania bara ndani ya wilaya 44.

Katika hatua nyingine Profesa Mgaya ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha zaidi za utafiti katika maeneo ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria ili kuwezesha nchi kuendeleza kikamilifu tafiti zake hata baada ya wafadhili kumaliza muda wao.

Amewataka wataalam wa maabara nchini kujituma na kujifunza matumizi mapana zaidi ya mashine za GeneXpert zilizopo katika hospitali mbalimbali ili kuhakikisha kuwa zinatumika pia katika kupima Virusi Vya Ukimwi kwa watanzania wakiwemo watoto na siyo Kifua kikuu tu kama ilivyotambulika hapo awali.

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Prof. Yunus Mgaya

No comments: