NMB yafanya mapinduzi makubwa ya malipo nchini
Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya Mastercard imezindua matumizi ya kadi za kisasa zaidi za kieletroniki ambazo zinatarajiwa kuwa chachu ya mapinduzi makubwa ya malipo nchini, na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu wengi.
Kadi hizo zinazowezesha malipo ya kabla (prepaid card) na malipo kwa mkopo (credit card) zimezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam katika hafla iliyoshuhudiwa na wadau mbalimbali akiwemo Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Bernard Kibesse, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa viongozi wa benki hiyo, ushirikiano na Mastercard kutoa huduma hizi mbili utakuwa wa manufaa mengi na mafanikio makubwa si kwa wateja wa NMB tu bali pia kwa sekta ya kifedha na Watanzania wote kwa ujumla.
Hii inatokana na kadi hizi kuweza kutumiwa na wateja na wasio wateja wa NMB ambayo huduma zake zinapatikana nchi nzima kutokana wigo mpana wa matawi zaidi ya 220, mawakala zaidi ya 7000 na mapinduzi ya huduma za kibenki kwa kutumia njia mbadala za kidijitali kama vile NMB Mkononi.
Katika mkakati wake wa kutoa huduma kupitia kadi za kielektroniki za Mastercard ambazo pia zina uwezo wa kutunza fedha, kufanya malipo kwa intaneti au kwenye point of sales (POS), Benki ya NMB imepanga kuzisambaza kwa zaidi ya watu milioni tatu ndani ya miaka mitano. Dkt. Kibesse alisema litakuwa jambo jema kama lengo hilo litakuwa maradufu ili huduma hii mpya iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo na uhakika wa Watanzania wengi kuwa na huduma za kibenki muda wote na mahali popote.
Naibu Gavana huyo pia alisisitiza umuhimu wa kadi hizo kusambazwa hadi vijijini na maeneo ya pembezoni kwa kuwa faida yake ni pamoja na kuwasaidia wakulima kujiwekea akiba hata kabla ya kufungua akaunti. Hilo likifanikiwa, alifafanua, Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa katika jitihada zake za kuwa uchumi usiotegemea malipo ya fedha taslimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema huduma ya kadi za malipo ya kabla na zile za malipo kwa mkopo ni moja ya miradi mikubwa ambayo taasisi hiyo imefanya na Mastercard. Mwaka 2015, washirika hao wawili walizindua Mastercard debit cards ambazo zimesambazwa kwa wateja zaidi ya milioni tatu.
Mradi wa pili ulikuwa ni uzinduzi wa Mastaboda ambayo inawawezesha waendesha pikipiki kupokea malipo kupitia simu za mkononi. Bi. Zaipuna alisema mradi huu mpya na wa tatu na Mastercard ni ushirikiano wa muhimu sana na wa faida kwa sekta ya fedha nchini na kwa Watanzania wote kwa ujumla.
Aidha, mpango huu unaenda sambamba na mkakati endelevu wa NMB wa kuwajumuisha wananchi wengi zaidi kwenye huduma za kibenki na kuwaingiza kwenye mfumo wa malipo kwa kadi. Pamoja na urahisi na usalama katika kufanikisha miamala, kadi hizi zitakuwa msaada mkubwa kwa wafanyabiashara ambao shughuli zao zinahitaji fedha za kigeni. Hatua hii ni muhimu sana kwa Tanzania na tunaamini itaongeza tija na thamani kwa wateja wetu kuanzia makampuni mpaka wateja binafsi.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Uendelezaji Biashara wa Kampuni ya Mastercard Afrika Mashariki, Frank Molla, alisema ubia wa kampuni hiyo na NMB ni sehemu ya mkakati wao wa kuwafikia watu bilioni moja duniani na kuwaingiza kwenye uchumi wa kidijitali mpaka ifikapo mwaka 2025.
Naibu Gavana wa Benki ya Tanzania, Dk. Bernard Kibesse (Katikati) akimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Dkt. Edwin Mhede baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kadi za NMB Prepaid na NMB Credit. Wakishuhudia kutoka kushoto ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha, Benedict Baragomwa.
Hizi ndizo aina ya kadi mpya za NMB Prepaid (Nyekundu) na NMB Credit.
No comments: