MPANGO WA ELIMU BILA MALIPO WAZINUFAISHA SHULE 156 SERENGETI
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Serengeti, Amsabi Jeremia Mrimi, kwenye mkutano wa kampeni uliyofanyika, katika viwanja vya Sokoine, wilayani Serengeti, Septemba 19, 2020. Katikati ni Diwani wa Kata ya Mkanwa, Mwita Mapancha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiteta jambo na Mgombea Ubunge wa jimbo la Serengeti, Amsabi Jeremia Mrimi, katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika viwanja vya Sokoine, Mugumu Serengeti, Septemba 19, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Wananchi wa jimbo la Itilima, wakimshangilia Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia, katika mkutano wa kampeni uliyofanyika katika Kata ya Ligangabilili, Septemba 19, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***************************************
SHULE 156 za wilaya ya Serengeti zikiwemo 122 za msingi na 34 za sekondari zimenufaika na mpango wa elimu bila malipo kwa kupatiwa sh. bilioni 6.2 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Hayo yamebainishwa jana jioni (Jumamosi, Septemba 19, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mugumu, wilayani Serengeti, mkoani Mara katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Sokoine.
Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya miaka mitano, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 2.9 zilitolewa kwa shule za msingi 122 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.3 zilitolewa kwa shule 34 ili kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.
Akielezea mpango mwingine ambao umezinufaisha shule nyingi za wilaya hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alisema mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa tangu 2015 hadi 2020 umewezesha sh. bilioni 2.7 zitolewe kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za walimu wa shule za msingi.
“Shilingi bilioni 1.7 zilizotolewa awali na awamu ya pili zikatolewa shilingi bilioni moja. Baadhi ya shule za msingi zilizonufaika na fedha hizo ni Wageti, Nyamakendo, Moningori, Masangura, Maburi, Kitunguruma, Itununu, Mchuri, Merenga, Mesanga, Miseke, Busawe, Musati, Monuna, Nyamburi, Nyiberekera, Motukeri, Kemugongo, Nyansurumunti, Mugumu na Nayaigabo,” alisema.
Alisema shule za sekondari zilipatiwa sh. milioni 3.076 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule ikiwemo maabara, madarasa, mabweni na vyoo. “Katika awamu ya kwanza zilitolewa shilingi bilioni 2.1 na awamu ya pili zikalipwa shilingi milioni 976.2.”
Alizitaja shule hizo kuwa ni Mugumu, Kitunguruma, Busawe, Nyamoko, Natta, Robanda, Serengeti, Ring’wani, Machochwe, Rigicha, Manchira, Mama Maria Nyerere, Ikongoro, Nagusi, Dkt. Omari Ali Juma na Nyambureti.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia mkutano huo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli na kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Serengeti, Bw. Amsabi Jeremiah Mhimi, mgombea udiwani wa kata ya Stendi Kuu, Bw. Steven Mapancha na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Serengeti.
Kuhusu maji safi na salama, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.4 zimetumika kukarabati na kujenga miradi mbalimbali wilayani Serengeti, ikiwemo vijiji vya Natta, Motukeri, Makundusi, Nyamakobiti, Majimoto, Musati, Kebanchabancha, Kutunguruma, Kenyana na Nyamitita.
“Vilevile, shilingi milioni 62.5 zimetumika kwa ajili ya uchimbaji wa kisima kimoja kwenye kijiji cha Makundusi na ukarabati wa visima vya pampu za mikono kwenye vijiji 19,” alisema.
Kuhusu huduma ya umeme, Mheshimiwa Majaliwa alisema jumla ya vijiji 69 kati ya vijiji 78 vya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti vimepata umeme na vijiji vilivyobaki visivyo na umeme ni tisa tu ambavyo vitapata kwa sababu mkandarasi yuko kazini.
No comments: