MLOGANZILA YASHIRIKI HUDUMA YA UCHUNGUZI WA AFYA PAROKIA YA KIBABMBA
Daktari Bingwa wa pua, masikio na koo Godlove Mfuko wa Hospitali ya Mloganzila akimfanyia uchunguzi wa masikio Mwananchi aliyefika kupata huduma.
Mfamasia wa Muhimbili-Mloganzila Sista Maria Mumelo akiwaelekeza wateja matumizi sahihi ya dawa.
Mtaalamu wa usikivu Theresia Uiso (kulia) akimpima mgonjwa kiwango cha usikivu.
Wananchi mbalimbali waliojitokeza kupima afya zao katika Parokia ya Kibamba wakisubiri kupata huduma.
Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakati akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo Parokia ya Kibamba jijini Dar es salaam.
Waumini wa Parokia ya Kibamba wakisikiliza hotuba wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo.
Dkt. Julieth Magandi (kushoto) akiwasha mshumaa kama ishara ya upendo na kuzindua huduma ya upimaji wa fya bure kwa wananchi.
……………………………………………………………
Wananchi wamehimizwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kupata tiba kwa wakati na kujikinga na maradhi mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa leo jjijini Dar es salaam na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakati akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Prof. Lawrence Museru katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo Parokia ya Kibamba.
Dkt. Magandi amesema unapopima afya na kugundua tatizo mapema utapata tiba kwa wakati na kuepuka athari zinazoweza kujitokeza unapochelewa kupata huduma.
“Nawasihi waumini wa kanisa hili na wanachi wote kwa ujumla tutumie fursa hii kupima afya kwani kinga ni bora kuliko tiba, ugonjwa unapogundulika mapema utapata tiba kwa wakati, vilevile ukiwa na afya njema utaweza kushiriki katika shughuli za maendeleo kwani maendeleo hujengwa na watu wenye afya bora”amesema Dkt.Magandi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha kisukari na magonjwa yasiyoambukiza Prof. Andrew Swai amewasihi wananchi kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi , kupunguza matumizi ya chumvi kwa wingi , mafuta pamoja na sukari ili kuepuka maradhi yasioambukiza kama Kisukari na shinikizo la damu.
Naye Paroko – Padri Prejo Joseph ameeleza kuwa Parokia ya Kibamba inasheherekea kumbukumbu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya afya kwa umma, kupima afya bure kwa magonjwa ya macho, masikio, pua na koo, afya ya kinywa na meno, kupima Virusi vya Ukimwi, ushauri nasaha, huduma za afya kwa watoto, saratani ya matiti, tezi dume, saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kuchangia damu.
Paroko Joseph ameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kutoa wataalamu wake ikiwemo madaktari bingwa katika kufanikisha zoezi la upimaji wa afya bure.
No comments: