KAIMU KAMISHNA WA UHIFADHI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI TANZANIA TAWA BW. MABULA MISUNGWI AMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA RUKWA.
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Bw. Mabula Misungwi Nyanda, amekutana na kufanya kikao na Mkuu wa Mkoa Rukwa. Bw. Joachim Wangabo, mnamo tarehe 25.09.2020. Katika kikao hicho, Kaimu Kamishna alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa lengo la ziara yake ni kujitambulisha kwake akiwa ni mdau muhimu kutokana na TAWA kusimamia Mapori ya Akiba mawili ndani ya Mkoa huo.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Rukwa. Kwa upande wa TAWA, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi aliambatana na Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Bw. Sylvester Mushy, Kaimu Kamishna Msaidizi Mwandamizi Kanda ya Kusini Bw. Pascal Mrina, Meneja wa Pori la Akiba Uwanda Bw. Orest Njau, Mkuu wa Kanda wa Pori la Akiba Lwafi Bw. Asubuhi Kasunga, Afisa Mhifadhi Dawati la Miundombinu Bw. Noti Mgaya, Fundi Sanifu Mwandamizi Bw. Jafari Sozi na Afisa Habari Bw. Beatus Maganja.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa alielezea kufarijika kwake kwa ujio wa Kamishna wa Kamishna TAWA, kutokana na kuwepo kwa baadhi mambo ambayo Kamishna anaweza kuyafuatilia na kuchukua hatua. Aidha, alitumia nafasi hiyo kumweleza Kamishna wa Uhifadhi kuhusu shughuli za uhifadhi katika Mkoa huo ambapo alibainisha kuwepo kwa changamoto kadhaa katika Mapori ya Akiba ya Lwafi na Uwanda ambayo yapo katika Mkoa wa Rukwa. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na; uvuvi haramu, uvamizi wa mifugo, kilimo na miundombinu duni katika Pori la Akiba Uwanda, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu uhifadhi, ujangili hususan wa mbao, mgogoro wa matumizi ya ardhi na uharibifu wa alama za mipaka katika Pori la Akiba Lwafi.
Aidha Mkuu wa Mkoa amemuagiza Kamishna wa Uhifadhi kuangalia uwezekano wa kutekeleza masuala yafuatayo; kutenganisha usimamizi wa pamoja wa Mapori ya Akiba ya Rukwa na Lwafi, Kuunda kikosi cha kuthibiti wanyamapori wakali na waharibifu, kuimarisha doria za anga kwenye maeneo ya ziwani na nchi kavu, kuendelea kuweka alama za vigingi kwenye mipaka ya hifadhi ili kupunguza migogoro, kuwaunganisha watumishi wa Halmashauri na TAWA katika kulinda rasilimali za wanayamapori pamoja na kuboresha vitendea kazi katika Mapori ya Akiba yaliyopo kwenye Mkoa huo.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Uhifadhi alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ukaribisho wake na akatumia nafasi hiyo kumwelezea kuhusu muundo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Taasisi za Uhifadhi zilizopo chini ya Wizara hiyo pamoja na majukumu ya kila Taasisi ili kuwa na uelewa wa pamoja.
Aidha, Kamishna wa Uhifadhi alijikita zaidi kuielezea TAWA, tangu kuanzishwa kwake, maeneo inayosimamia pamoja na malengo yake ya; ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, kutoa huduma ya kuridhisha kwa wateja wake pamoja utendaji wenye tija na ufanisi.
Kamishna wa Uhifadhi alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa ameyapokea maelekezo yake yanayohusiana na shughuli za uhifadhi ndani ya Mkoa huo na kuahidi kuyatekeleza. Alikiri kuwepo kwa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kwenye Mkoa huo na maeneo mbalimbali nchini akitolea mfano baadhi ya Wilaya za Itilima, Bunda na Tunduru na kusema kuwa Wizara kwa kushirirkiana na wadau imeandaa Mkakati kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibu ambapo miongoni mwa mbinu zinazopendekezwa kwenye Mkakati huo ni kuunda vikosi vya pamoja kama alivyoshauri Mkuu wa Mkoa. Alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa Mkakati huo utakapokamilika utasamabazwa kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji. Pia aliwaagiza viongozi wa Mapori ya Akiba yaliyopo ndani ya Mkoa wa Rukwa kufanya kazi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa pamoja na wananchi ili kuwezesha uhifadhi endelevu.
Aidha, Kaimu Kamishana wa Uhifadhi aliwasilisha ombi kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu ushirikiano kati ya TAWA na Uongozi wa Mkoa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Mapori yaliyopo ndani ya Mkoa huo. Alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa sasa TAWA inatekeleza miradi miwili ya (i) Ujenzi wa ghala la silaha unaotekelezwa na SUMA JKT ambao umekamilika mwezi Agosti, 2020 (ii) Mradi wa ujenzi wa nyumba mbili (2) za watumishi zinazojengwa na Kampuni ya Samalanga General Enterprises ambao umekwama kutokana na mkandarasi kukiuka mkataba wa makubaliano. Miradi yote hiyo inatekelezwa katika Kijiji cha Kipeta yalipo Makao Makuu ya Pori la Akiba Uwanda. Kaimu Kamishna amemwomba Mkuu wa Mkoa ushirkiano wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kusaidia kupatikana kwa mkandarasi huyo.
Mkuu wa Mkoa alikubali na kupokea ombi hilo, kisha akaviagiza vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo TAKUKURU kuanza ufuatiliaji wa suala hilo. Aidha, alimwagiza Kamishna wa Uhifadhi kuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye vituo vilivyopo ndani ya Mkoa huo, ni vyema uongozi wa Mkoa ukashirikishwa.
Mwisho Mkuu wa Mkoa alimshukuru tena Kaimu Kamishna wa Uhifadhi na washiriki wote na kuagiza utelezaji wa yale yaliyoahidiwa ufanyike kwa wakati.
No comments: