JUMUIYA YA ULAYA YATAKIWA KUONDOA VIZUIZI VYA KUSAFIRI
Mkutano maalum wa mashauriano ukiongozwa na Mheshimiwa Balozi Nyamanga kwa upande wa OACPS (kulia) na Mheshimiwa Waziri Muller akiongoza ujumbe wa Ujerumani (kulia).
Mhe. Balozi Nyamanga akiendesha kikao hicho cha mashauriano. Kulia ni Balozi wa Togo Mhe. K. Mbeou na kushoto ni Katibu Mkuu wa OACPS Balozi Dkt Chikoti.
…………………………………………………………………
Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS) imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuondoa vizuizi vya kusafiri (travel bans) kwa baadhi ya nchi za OACPS hususan zile zilizoonesha kuwa salama zaidi dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Corona kama Tanzania. Wito huo ulitolewa katika kikao maalum cha mashauriano baina ya Jumuiya ya nchi za OACPS na nchi ya Ujerumani ambayo kwa sasa ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya.
Mashauriano hayo yaliyofanyika tarehe 9 Septemba 2020 katika Ofisi za Jumuiya ya OACPS, Brussels nchini Ubelgiji, yaliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS walioko Brussels, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na ujumbe wa Ujerumani uliongozwa na Waziri wa Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER.
Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kusimamia ithibati za tafiti za chanjo za ugonjwa wa Corona na Shirika hilo kuendelea kujengewa uwezo wa kusimamia utaratibu wa kuhakikisha kuwa chanjo itakayothibitika inawafikia mataifa yote kwa usawa na kwa gharama nafuu.
Kikao hicho kilijadili pia hatua mbalimbali zinazopaswa kuongeza msukumo kwa Umoja wa Ulaya katika kuzisaidia nchi za OACPS kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na ugonjwa wa Corona hususan katika sekta ya utalii na
kilimo. Mikakati iliyojadiliwa ni pamoja na ile inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya ulipaji wa madeni ya nchi za Jumuiya ya OACPS na wito wa nchi za OACPS kuutaka Umoja wa Ulaya kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na taratibu mpya za biashara zilizopangwa kuanza kutumika mwanzoni mwa mwaka ujao ili kuzipa nafasi nchi za OACPS kujipanga zaidi kabla ya kuanza kutumia kanuni hizo.
Kupitia mashauriano hayo, pande zote mbili zilitathmini mwenendo wa majadiliano ya Mkataba mpya wa ubia wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya OACPS na Umoja wa Ulaya yanayoendelea hivi sasa baada ya mkataba wa sasa kufikia kikomo mwezi Desemba 2020. Pande mbili zilijadili kwa kina namna ya kushirikiana katika maeneo yanayolenga kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo, uwiano ulio sawa katika biashara na maendeleo ya teknolojia katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu.
Kikao kilihitimishwa kwa Ujerumani kuonesha utayari wa kuyapa kipaumbele masuala yote yaliyojadiliwa katika kipindi cha uongozi wake wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi hiki ambacho inashika nafasi ya Rais wa Baraza la Mawaziri wa nchi 79 wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya na kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Ujerumani kwenye Baraza la Umoja huo wa Ulaya kusukuma ajenda zenye manufaa na maslahi kwa pande zote mbili.
No comments: