EMIRATES YAREJESHA ZAIDI YA USD BILIONI MOJA KWA WATEJA

SHIRIKA la ndege la kimataifa la Emirates limerejesha zaidi ya dola 1.4 bilioni kwa wateja waliopanga na kulipa tiketi kwa safari za maeneo mbalimbali duniani na kushindwa kusafiri kutokana na mlipuko wa janga la Corona (Covid-19.)

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa Emirates Tim Clark shirika hilo imeelezwa kuwa, maombi milioni 1.4 ya marejesho ya fedha yalikamilishwa tangu mwezi Machi ambayo ni sawa na asilimia 90 safari zilizoombwa na kupangwa, na hiyo ni majumuisho ya maombi ya wateja kote duniani hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni.

Imeelezwa kuwa tangu litokee janga la Corona shirika hilo limeendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali wakiwemo mawakala katika kuhakikisha wanarejesha fedha kwa wateja waliokata tiketi zao kupitia mawakala.

Katika taarifa hiyo Rais wa shirika hilo Tim Clark amenukuliwa akisema kuwa, " Tunaelewa na tumejizatiti kurejesha fedha za safari zilizopangwa na wateja wetu, lakini janga la Corona likaingilia kati,na tunawashukuru wateja wetu kwa kuwa waelewa na wavumilivu katika hili" ameeleza Tim.

Tim ameeleza kuwa hadi kufikia sasa tayari baadhi ya maeneo duniani yakiwemo masoko yamefunguliwa, na anga lipo wazi hivyo watahakikisha wanatoa huduma salama, ya uhakika na ya kufurahia kwa wateja wao.

Amesema kuwa sera za kupanga safari kwa wateja  zimeboreshwa zaidi hasa kwa kuzingatia usalama kwa wateja kupitia shirika hilo la kimataifa.

Hadi sasa Emirates inatoa huduma za safari mwa miji zaidi ya 80, ukiwemo mji wa Dubai ambao tayari umefunguliwa kwa biashara za kimataifa na utalii na mapumziko na kwa wasafiri wote watakaowasili hapo vipimo vya Covid-19 ni lazima bila kujali ni wapi wametoka.

Imeelezwa kuwa Dubai kama ilivyo Tanzania ambayo il ilikuwa kituo cha kwanza kuanza safari salama katika nyanja ya utalii baada ya Covid-19, shirika hilo litaendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha usalama kwa wateja.

Shirika hilo limewatoa hofu wateja wake na kuwahakikishia usalama wa hali ya juu pindi watumiapo usafiri wa Emirates kufurahia safari zao za kibiashara, mapumziko na utalii katika vituo mbalimbali ikiwemo Dubai ambayo kwa mwaka 2019 pekee ilipokea watalii milioni 16.7 na kuendesha maelfu ya mikutano na maonesho pamoja na shughuli za burudani.

No comments: