DK.JOHN MAGUFULI AWATAKA WANANCHI CHATO WAKUMBUKE WALIVYOTOKA NAYE MBALI KUANZIA UBUNGE HADI URAIS


Na Said Mwishehe, Michuzi TV- Chato

RAIS Dk.John Magufuli ambaye kwa sasa anaendelea na mikutano ya kampeni za kuomba ridhaa kwa Watanzania kumpa miaka mingine mitano kuongoza nchi amekumbusha maelfu ya Wana Chato jinsi alivyoanza historia yake ya safari ya uongozi.

Dk.Magufuli amekumbusha historia hiyo ya safari yake ya uongozi wakati anazungumza kwenye mkutano wake wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu uliofanyika wilayani Chato mkoani Geita.

Amesema mwaka 1995 alikuja kuomba kura  kwa nafasi ya ubunge akapata, akaomba tena mwaka 2000 akapata, mwaka 2005 na mwaka 2010 pia akaendelea kuwa mbunge wao.

 "Mara mbili mmenipitisha bila kupingwa, sikupingwa na chama chochote, miaka 10 niligombea na miaka mingine 10 nilipita bila kupingwa.Katika miaka 20 ambayo mnilinichagua nimejifunza mengi, na ninyi ndio mlifanya wengine wanijue.

"Mwaka 2015 chama changu kinanipa dhamana ya kupeperusha bendera ya nafasi ya urais, nawashukuru kwa kunipa nafasi ya kuongoza kwa miaka mitano na leo nimekuja kuomba tena.Kazi ya urais sio nyepesi lakini nafahamu katika kipindi cha miaka 20 ya ubunge na miaka mitano ya urais nimejifunza mengi.

"Nimeijua Tanzania yote, najua matatizo yao, na ndio maana ninaomba nafasi ya urais nipeni hii kazi nikafanye kama mtumishi wenu na nimekuwa mtumishi wa kweli.Mambo yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano ni mengi, sana,"amesema Dk.Magufuli.

Amewaambia wananchi wa Chato kwamba hata shule ya sekondari ya chato haikuwa hivyo, hata ukuta haukuwepo na kwamba wakati anachaguliwa kuwa mbunge ilikuwa inaitwa Biharamuro Magharibi, haikuwa wilaya lakini leo ni wilaya.

"Nimesimama hapa kama mtumishi wenu, nchi yetu inachangamoto nyingi, kuongoza ni kuongozwa pia, kuongoza panahitaji upendo, hekima na busara.Kama taifa katika miaka mitano tumekutana na changamoto nyingi, za kiuchumi, kiusalama lakini tumeungana kuhakikisha tunaleta mabadiliko katika nchi yetu,"amesema.

Dk.Magufuli amesema wamefanya kwa miaka mitano na leo wanasimama tena kuomba tena miaka mitano mingine wakafanye makubwa zaidi.

"Maajabu tutayafanya kweli, kila kijiji, kila mkoa kuna jambo linafanyika, hata dar kuna madaraja ya maghorofa, tunaitengeneza nchi kuwa ya kisasa, ndio maana tunaomba tena miaka mitano.

Hata hivyo amesema maendeleo yamefanyika maeneo yote nchini. "Halafu mtu anazungumza nimejenga uwanja nyumbani, nikifa nitaenda nao kaburinii, lazima uwe na mipango mipana, tunajenga viwanja vya ndege 11, hivyo vyote hawaoni wanaona cha Chato tu, washindwa na wakalegee.

 "Na hiyo ndio mipango, wapo watu ambao hawapendi ufanye chochote, tumenunua ndege mpya 11, utalii umepanda, mtu anasimama ameshiba ugali, huko alikotoka amekuja na bajaji, mambo mengine yanaudhi, hawa watanzania wanafahamu walikotoka, waliko na wanakokwenda, ndiomaana nimesimama hapa kuwakumbusha ili tusiuziwe mbuzi kwenye gunia.

"Ni lazima sisi watanzania na watu wa Chato tutambue tulipokuwa na tunakokwenda, wakati naingia barabara ilikuwa ya vumbi, leo unaweza kutoka Chato mpaka Mtwara bila kukanyaga vumbi.Mimi ni mtumishi wenu, kama kwa miaka 10 mlinipitisha bila kupingwa, mwaka huu asitokee hata mtu mmoja akapoteza kura,"amesema.

 Dk.Magufuli ametumia nafasi hiyo kueleza kila akimfikiria Benjamin Mkapa moyo wake unamuuma."Nami nimeokotwa na mkapa huku jalalani, Mkapa ndio alinipa nafasi, maana siku hizi kuna msemo ukipewa kazi na Magufuli unaambiwa umeokotwa jalalani."

Maelfu kwa maelfu ya wananchi wakiwa katika Uwanja wa Mazaina mjini Chato mkoani Geita kumsikiliza mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Hicho Tawala na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika mkutano wa hadhara wa kampeni leo Jumatatu Septemba 14, 2020

No comments: