DAWA ZA KULEVYA ZAMPELEKA MALITIKA MIAKA 30 JELA
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi imemuhukumu mfanyabiashara Said Malikita kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.
Hukumu hiyo imesomwa na Jaji Lilian Mashaka wa mahakama hiyo Septemba 18, 2020.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mashaka amesema, upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake nane waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi na vielelezo vitano vilivyowasilishwa wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa.
"Baada ya kuchambua ushahidi, upande wa Jamuhuri, wameweza kuthibitisha kesi bila kuacha shaka hivyo mahakama inakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela". Amesema Hakimu Mashaka
Mapema kabla ya kusomwa adhabu hiyo, Hakimu Mashaka aliuliza upande wa Jamuhuri kama walikuwa na lolote la kusema ambapo wakili wa serikali Constantine Kakula alisema hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa ila ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo kwani vitendo vya makosa ya dawa za kulevya vimekithiri katika jamii.
Aidha mshtakiwa katika utetezi wake ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwani ana watoto wadogo ambao bado hawajaenda shule, ana wazazi wanaomtegemea, baba yake ni mzee wa miaka 84 na mama yake licha ya kuwa ni mzee pia ni mgonjwa sana na hajamuona tangia alipoingia gerezani 2017.
Katika kesi ya msingi inadaiwa Agosti 29,2017 huko katika mtaa wa Ufipa eneo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na gramu 238.4 za dawa za kulevya aina ha Heroine Hydrochloride .
No comments: