Aliyelazwa wodini Muhimbili siku 490 aruhusiwa kurudi nyumbani
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (Upanga) imemruhusu Daudi Mikidadi (17) kutoka hospitalini kwenda anakoishi ambapo ataendelea kutumia mashine maalumu ya kumsaidia kupumua (oxygen concentrator).
Mikidadi ni kijana yatima kutoka Kituo cha Kurasini Children’s Home ambaye alilazwa Hospitalini hapo Aprili 20, 2019 ambapo aliingia wodini akiwa na miaka 16 na kutoka leo akiwa na miaka 17 alikuwa anaumwa sana na kushindwa kupumua vizuri hivyo kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua.
Baada ya kufanyiwa uchunguzi Mikidadi aligundilika kuwa mapafu yake yote mawili yameharibika kutokana na kuugua ugonjwa mmoja wapo wa mapafu (ugonjwa umehifadhiwa). Hivyo atahitaji usaidizi wa mashine ya kupumulia kwa maisha yake yote au kupandikizwa mapafu yote mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuruhusiwa mgonjwa huyo, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya Umma wa hospitali hiyo Aminiel Aligaesha amesema watalamu wameridhika kwamba hali aliyonayo mgonjwa sasa, anaweza kurudi kwenye kituo chake ambapo Hospitali ikishirikiana na kituo hicho wameandaa chumba maalumu chenye umeme na mahitaji mengine muhimu kwa ajili yake.
"Hospitali ya Taifa Muhimbili imegharimia matibabu yake yote, imempa msaada wa mashine ya kumsaidia kupumua (oxygen concentrator), Madaktari walioko kwenye mafunzo kwa njia ya vitendo (Intern Doctors) wamechanga na kumnunulia mtungi wa oksijeni tiba, kuna msamaria mwema mwingine amempa msaada wa mashine ndogo ya kupumulia (portable oxygen machine)". amesema Aligaesha.
Ameongeza kuwa, sehemu ya vifaa hivyo vitamsaidia akiwa nje ya chumba chake pale umeme utakapokatika au akiwa na safari yeyote na wakati akiwa anaenda kuhudhuria kliniki mbalimbali au kufanyiwa vipimo mara kwa mara kama mazoezi tiba n.k.
Mikidadi amelazwa Hosptalini hapa kwa siku 490, kati ya hizo siku 127 amekaa kwenye wodi ya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU). Hospitali inatoa wito kwa wasamaria wema kutembelea kituo anachoishi Mikidadi ili kuendelea kumsaidia kwa mahitaji mbalimbali.
No comments: