Waziri wa TAMISEMI akabidhi bilioni zilizookolewa Njombe


Na Amiri Kilagalila, Njombe
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewaonya wale wote watakaojaribu kutumia vibaya fedha za wananchi zilizokusanywa toka kwa wadaiwa sugu wa iliyokuwa benki ya wananchi Njombe Njocoba na vyama vya ushirika.

Kauli ya Jafo imetolewa wakati akikabidhi hundi ya zaidi ya shilingi bilioni 5 fedha zilizokusanywa toka kwa wadaiwa sugu mkoani Njombe na kwamba hatarajii kuona fedha hizo zinatumika tofauti na matarajio ya wananchi wenye fedha zao.

“Nimshukuru sana ndugu yangu Ole Sendeka aliyekuwa mkuu wa mkoa huu wa Njombe,kwa hii kazi kubwa aliyoifanya na wenzake (ya ukusanyaji wa fedha zilizotaka kutafunwa na wachache) niwapongeze wote.Kazi iliyofanyika ni kubwa zaidi ya fedha zote bilioni 16, bilioni 5.048 zimeokolewa katika mkoa mmoja wa Njombe.” Alisema Jafo

“Nakushukuru sana mtendaji mkuu,mkurugenzi wa TAKUKURU Taifa ulivyoweza kusimamia urudishaji wa fedha katika maeneo mbali mbali.Leo hii zaidi ya shilingi bilioni 16 zimeshaludi kwa Watanzania.”Alisema Waziri wa TAMISEMI Seleman Jafo

Awali mkurugenzi wa taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini Tanzania Brigedia Generali John Mbungo amesema mkoa wa Njombe umefanikisha kuokoa fedha nyingi zaidi kuliko mikoa mingine huku wakiendeleza oparesheni ili fedha zote zirejeshwa kama Rais alivyoelekeza.

Aidha Generali John Mbungo ameendelea kuonya kujihusisha na maswala ya Rushwa katika kipindi hiki cha Uchaguzi.

“Nchi yetu inaingia katika zoezi la uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani utakaofanyika Octoba 28,2020 kote nchini.Ninawaomba wagombea na wapiga kura kuzingatia sheria,kanuni na taratibu za nchi wakati wa kampeni na tufanye kampeni za kistaarabu bila kushiriki katika matendo ya Rushwa yanayodharirisha utu wa Mtanzania.” Mkurugenzi wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Nchini Brigedia Generali John Mbungo

Baadhi ya wakazi wa Njombe akiwemo mwenyekiti wa soko mzee Akan Kyando wameonesha kufurahishwa na kazi kubwa iliyofanyika na serikali ya awamu ya tano katika miradi ya maendeleo.

Waziri Jafo akiwa mkoani Njombe amezindua mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi katika mji wa Njombe yaani master plan,kuweka jiwe la msingi katika soko kuu jipya pamoja na kukabidhi hundi ya zaidi ya shilingi bilioni tano fedha zilizookolewa toka kwa wadaiwa sugu wa iliyokuwa benki ya wananchi Njombe Njocoba Sacco's na Amcos.

No comments: