WAZIRI WA NISHATI AMPONGEZA MENEJA WA TANESCO ARUSHA, AMPA MAAGIZO
Na Woinde Shizza,Michuzi TV Arusha
WAZIRI wa Nishati Dkt Medard Kalemani amepongeza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha Mhandisi Herin Muhina kwa kazi nzuri anayoifanya huku akimwagiza ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa awe amekamilisha kazi ya kupeleka umeme katika mitaa yote iliyo pembezoni mwa Mji.
Aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akifanya ziara ya kikazi ndani ya Halmashauri ya Wilaya Arusha ambapo alifanikiwa kutembelea na kuwasha umeme katika shule mbili za shule ya sekondari ya Moivaro na shule ya sekondari ya Nyahiri Iliopo ndani ya kata ya Terrat.
Dk.Kaleman amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo ya aina hiyo nchini kote kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kama ilivyo kwa vijijini.
Amesema amefurahishwa na Uongozi wa Shule ya Sekondari Moivaro kuona umuhimu wa kulipia gharama za kuunganishiwa umeme na kupata huduma hiyo, ikiwa na mwaka mmoja tu tangu ianzishwe.
Ametoa rai kwa viongozi wengine katika maeneo mbalimbali nchini, kuiga mfano huo kwa kuhakikisha taasisi zote za umma zinapewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ili kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi.
Aidha amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 103.8 kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa majiji, mikoa, manispaa na miji, nchi nzima.
Ameongeza Serikali ilikaa ikaona maeneo hayo yaliachwa kwa kipindi Cha muda mrefu bila kuwa na miundombinu ya umeme, wakaona wawapunguzie gharama kutoka walivyokuwa wanalipa zamani shilingi 177,000 na katika baadhi ya maeneo 380,000 hadi shilingi 27,000 tu.
Kwa upande wa Wilaya ya Arusha, Waziri Kalemani amesema kwamba kuna mitaa takribani 26 iliyo pembezoni mwa Mji na Serikali ilianza kuipeleka umeme kutoka mwaka 2018.
Kuhusu wananchi kulipia nguzo ili waunganishiwe umeme, amefafanua kuwa msimamo wa Serikali ni marufuku mwananchi kuuziwa nguzo na kuwataka wananchi atakaeuziwa atoe taarifa sehemu husika ikiwepo polisi.
Amewataka wananchi kuendelea kulipia huduma ya umeme pasipo kusubiri nguzo akisema hilo siyo jukumu lao kwani swala la nguzo aliwahusu
Katika hatua nyingine, Waziri aligawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wao kwa Taifa kupitia kazi wanayoifanya katika kuhabarisha na kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali, yakiwemo ya sekta ya nishati.
Aidha, aligawa vifaa hivyo kwa shule alizoziwashia umeme pamoja na walimu wake huku akielekeza kuwa vitumike kuwaunganishia umeme wa gharama nafuu ambao haulazimu kutandaza mfumo wa nyaya katika jengo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji, amempongeza Waziri Kalemani kwa uchapakazi katika kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kote, wanapata huduma ya umeme.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akimpa maelekezo Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Herin Muhina Juzi alipokuwa katika ziara yake.
No comments: