WANANCHI ILAKALA WATOA YA MOYONI KUHUSU MISITU YA ASILI INAYOWAZUNGUKA, WAPELEKA OMBI KWA TFCG

 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ilakala wilayani kilosa mkoani Morogoro wakiwa kwenye kikao maalumu ambacho kilikutana kwa ajili ya kuzungumzia namna ambavyo wanaweza kunufaika na uwepo wa misitu ya asili kwenye kijiji hicho.
 Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilakala wilayani Kilosa mkoani Morogoro Moshi Kihiki akizungumza na waandishi wakati wa kikao hicho ambacho pamoja na mambo mengine kilijikita kuzungumzia umuhimu wa uhifadhi wa misitu ya asili na namna wanavyoweza kunuifaika nayo kama ilivyo kwenye vijiji vingine.
 Mkurugenzi huyo, Ofisa Sera na Majadiliono kutoka MJUMITA Elida Fundi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mmoja ya msitu wa asili uliopo wilayani Kilosa.
 Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Ilakala wakiwa mkutanoni.
Ofisa Uhusiano wa TFCG Bettie Luwuge akiwa katika moja ya msitu wa asili uliopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro baada ya kwenda kukutana na wananchi wanaotekeleza mradi uhifadhi wa misitu ya asili.

Na Said Mwishehe, Michuzi TV.

WANANCHI wa Kijiji cha Ilakala wilayani Kilosa mkoani Morogoro wamesema wanatamani kunafaika na uwepo wa misitu ya asili inayowazunguka kama ilivyo kwa vijiji vingine vya Ulaya Mbuyuni, Kitunduweta, Muhenda na Ihombwe ambavyo vinatekeleza mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa nchini.

Wakizungumza kwenye mkutano maalumu wa kijiji uliohusisha pia baadhi ya maofisa kutoka Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania(TFCG) pamoja na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)wamesema wenzao ambao wana mradi huo wamekuwa wakipata manufaa makubwa yakiwemo ya kupata fedha zinazowasaidia katika kuwaleta maendeleo.

Akifafanua zaidi Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilakala kilichopo kata ya Muhenda wilayani Kilosa mkoani Morogoro Moshi Kihiki amesema vijiji ambavyo vinatekeleza mradi wa TTCS wamekuwa na maendeleo makubwa kiuchumi na kijamii.

Mradi huo wa TTCS unatekelezwa na TFCG) na MJUMITA), kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC) na umekuwa na manufaa makubwa kwa vijiji mbalimbali ambavyo vimebahatika kupata mradi huo ambapo Kihiki amesisitiza wanaona wivu kwa jinsi wenzao wanavyopata maendeleo huku wao wakishuhudia na hivyo ametoa ombi ili nao wawe na mradi huo.

"Ni matumaini yetu tukiwa na mradi huu tutaondoa changamoto nyingi tulizonazo kijijini kwetu.Kwa sasa kila ambacho tunataka kukifanya kwa ajili ya maendeleo yetu lazima tuchangishane lakini vijiji ambavyo vinamradi huo wanapohotaji kufanya jambo la maendeleo wanachukua fedha za kijiji ambazo zimepatikana kupitia mradi,"amesema Mwenyekiti huyo na kuungwa mkono na wananchi wenzake.

Ametoa mfano kuwa vijiji ambavyo vinatekeleza mradi huo unatokana na Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) baada ya kupata elimu kupitia TTCS wamekuwa wakijenga madarasa, zahanati, nyumba za watumishi pamoja na hata kukata bima ya afya kwa wananchi wote kwenye vijiji hivyo.

Hivyo amesema nao wanahitaji kupata mradi wa TTCS ili waanze kunufaika na rasilimali za misitu ambazo zimewazunguka kwenye kijiji chao cha Ilakala.

Mjumbe wa Serikali Kijiji Zuberi Kiokoteke, ameongeza kwamba bado kipo nyuma kwa maendeleo ukilinganisha na vijiji vingine, hivyo tumaini lao ni kupata mradi wa TTCS kisha na wao waanze kupata maendeleo.

Kwa upande wake John Mtimbanjayo ambaye ni Ofisa Maliasili wa Wilaya ya Kilosa ametumia nafasi hiyo kueleza Wilaya yao kwa sasa inao mkakati wa kusambaza dhana ya USMJ katika vijiji vyote vyenye misitu ya asili na kijiji cha Ilakala ni miongoni mwao.

Hata hivyo amesema uwepo wa mradi wa TTCS kwa kipindi cha miaka saba umeleta tija na mafanikio lukuki kwa wananchi ikiwemo ya kupata mamilioni ya fedha ambazo zimekuwa zikitumika kufanya maendeleo katika vijiji husika.

Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA Elida Fundi amesema waandishi wa habari ambao wamekuwa nao katika ziara ya kimafunzo wamepata nafasi ya kushuhudia mafanikio ambayo yamepatikana kwenye vijiji ambavyo vinatekeleza mradi, hivyo waliona ni vema wakaenda na kijiji ambacho hakina mradi ili kupata maoni ya wananchi.

"Mwamko wa vijiji kutekeza USMJ umekuwa mkubwa, ni jukumu la Serikali sasa kupitia halmashauri yake kutekeleza kwa vitendo USMJ kwa kuwa ina manufaa chanya.Waandishi wa habari mmewasikia wananchi ambao wanahitaji nao kunufaika na misitu yao ya asili na wanatamani wapate mradi huu,"amesema Fundi.


No comments: