WANACHAMA CCM, IGUNGA WASHAURIWA KUVUNJA KAMBI NA KUUNGANA PAMOJA KWA LENGO LA KUKIPATIA CHAMA USHINDI
Na Jumbe Ismailly, IGUNGA
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora wameshauriwa kuondoa tofauti na kuvunja kambi walizokuwanazo wakati wa kampeni za kura za maoani na badala yake waungane na kuwa kitu kimoja ili ushindi wa wagombea wa chama hicho uweze kupatikana kwa kishindo.
Ushauri huo umetolewa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Igunga kwa kipindi cha miaka kumi,Dkt Dalally Peter Kafumu wakati wa kuwatambulisha wagombea wa ubunge wa jimbo la Igunga,Nicholaus Ngasa na Seif Khamisi Gulamali wa jimbo la Manonga mara baada ya kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha Dkt Kafumu alifafanua kwamba ni ukweli usiopingika kwamba inawezekana kura za maoni zilikuwa zimewagawanyagawanya,lakini ni wakati muafaka sasa wa kuyasahau yaliyopita na wagange yajayo kwani hivi sasa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ni kimoja.
“Ninachowaomba wana Igunga sasa tumemaliza kura za maoni zinaweza kuwa zilitugawanyagawanya hebu tuyasahau sasa Chama Cha Mapinduzi ni kumoja na tutaanza kuanzia tarehe 28,tuwapige hawa jamaa wa upinzani tupate vijana wetu hawa waweze kuendeleza pale tulipofikia.”alisisitiza Dkt Kafaumu.
Hata hivyo mwakilishi huyo wa wananchi kwa vipindi viwili,pamoja na kuwahakikishia wanachama wa chama hicho furaha aliyonayo baada ya kukabidhi kipande cha eneo lake kwa kijana Ngasa,aliwataka wanachama hao washikamane ili serikali ya awamu ya tano iweze kufika inakotakiwa.
Akiwakabaidhi wagombea wa CCM fomu za kuomba kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,Msimaizi wa uchaguzi,Revocatus Kuul alisema kwamba jumla ya wagombea wa vyama vya siasa 11 walikwishakabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa.
Kwa mujibu wa Kuul ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga waliokabidhiwa fomu hizo katika jimbo la Igunga ni pamoja na Richard Nanyaro wa chama cha SAU,Edsoni Mlimba wa NRA,Frank Masunga CUF,Juma Khalfani Mremba wa UMD,Ngasa Ganja Mboje wa CHADEMA na Nicholaus George Ngasa wa CCM.
Kutoka jimbo la Manonga ni Majaliwa Kurwa wa ADC,Josephath Shilogile wa CHADEMA, Daudi Seleli wa CUF, Kasanga Maugaja wa ACT Wazalendo pamoja na Seif Khamisis Gulamali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakizungumza mara baada ya kupokea fomu kwa msimamizi wa uchaguzi,Mgombea wa ubunge jimbo la Manonga,Seif Khamisi Gulamali alitumia fursa hiyo kuwaomba wanachama na wanachi wa Igunga kwa ujumla wamuunge mkono mgombea wa jimbo la Igunga,Nicholaus George Ngasa ili aweze kuwatumikia kikamilifu.
Aidha Gulamali alisisitiza pia kwamba ili mwakilishi wa jimbo la Igunga asiwe na sababu za kujitetea atakapokwama kuwatumikia waliompa ridhaa katika jimbo hilo,aliwatahadharisha kwamba watakapokuwa wakichagua wagombea wasimchanganyie punda na ng’ombe kwani mambo hayataenda vizuri.
“Kwa hiyo tupo pamoja vijana mwenzangu mumuunge mkono nitafanyanaye kazi pamoja,tutashirikiana naye pamoja kwa hiyo mengi tutayazungumza kipindi cha kampeni,lakini hapa tulitaka kuwahakikishia kwamba mimi na Ngasa tupo kitu kimoja, tunajenga nyumba moja hatuna sababu ya kugombania fito.
Mgombea wa kiti cha Ubunge wa jimbo la Manonga,Seif Khamisi Gulamali akiwa amebebwa na wanachama wa chama hicho kuonyesha imani ya dhati kuwa wanamkubali kutokana na utekelezaji wa ahadi zake anazotoa kwa wananchi alipowasili kutoka ofisi za Tume ya Uchaguzi kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa.
Baadhi ya akina mama wa CCM waliohudhuria kwenye ofisi za chama hicho kuwapokea wagombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Manonga, Seif Khamisi Gulamali na jimbo la Igunga, Nicholaus George Ngasa wakionyesha furaha yao ya kuridhishwa na uteuzi uliofanyika katika majimbo hayo.
Wagombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Manonga, Seif Khamisi Gulamali(wa kwanza kutoka kushoto) na Nicholaus Geroge Ngasa wa jimbo la Igunga wakiwa kwenye ofisi za tume ya uchaguzi wakisubiri kupata maelekezo kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi, Revocatus Kuul.
(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
No comments: