TUME YAVIKUMBUSHA VYAMA VYA SIASA KUZINGATIA MAADILI YA UCHAGUZI WAKATI WA KAMPENI.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imevisihi Vyama vya Siasa kusoma na kuzingatia ipasavyo Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ili kuepuka usumbufu unaoweza kuwapata na kuathiri haki yao ya kufanya kampeni kwa ajili ya kunadi wagombea wao na kuelezea sera zao.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage wakati wa Mkutano kati ya Tume na Vyama vya Siasa uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu ajaulius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 01/08/2020.

Maadili hayo ya Vyama vya Siasa ambayo yalisainiwa kati ya Vyama vya Siasa, Tume na Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 27/05/2020 yana mambo ambayo yanatakiwa kufanya naambayo hayatakiwi kufanywa.

Jaji Kaijage alisema kuwa pamoja na mambo mengine, maadili yanavitaka Vyama vya Siasa kufanya kampeni za kistaarabu, kueleza na kunadi Sera na Ilani zao, na kuhamasisha hasa Wapiga Kura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

Aidha, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi alitaja baadhi ya mambo ambayo hayatakiwi kufanywa kwenye kampeni kuwa ni kuepuka kufanya fujo au kuchochea vurugu ya aina yoyote katika mikutano ya vyama vingine.

Zaidi ya hayo, Kaijage alisema Vyama vya Siasa havitakiwi kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi kijinsia, ulemavu, rangi au maumbile na kubeba silaha ya aina yoyote.

Kadhalika, Mwnywkiti wa Tume alizitaja Kamati Nne za Maadili ambazo zitasikiliza malalamiko dhidi ya Wagombea, Chama cha Siasa na Kiongozi wa Chama kilichovunja Maadili.

Kamati hizo za Madili ni Kamati ya Maadili Ngazi ya Kata ambayo itashughulikia Wagombea wa Udiwani,Kamati ya Maadili Ngazi ya Jimbo ambayo ni kwa ajili ya Wagombea wa Ubunge, Kamati ya Maadili Ngazi ya Taifa itakayoshughulikia Wagombea Kiti cha Rais na Makamu wa Rais na Kamati ya Rufaa itakayoshughulikia Rufaa za Wagombe wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais kama hatakubaliana na adhabu atakayopewa na Kamati ya Maadili Ngazi ya Taifa.

Baada ya Mkutano na Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iligawa vitabu saba (7) vya Maadili ya Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa vya mwaka 2020 kwa vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu, Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombe, Maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi, Maelekezo kwa Wasimamizi wa Vituo, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,Sura 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292 na kuvisihi kuvisoma na kuzingatia ipasavyo Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wakati wa kampeni..

Mwenyekiti wa Tume alivikumbusha vya vya siasa ratiba ya Uchaguzi kuwa uchukuaji Fomu za Uteuzi kwa Wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Raisi itakuwa tarehe 05/08/2020 mpaka tarehe 25/08/2020 na uchukuaji Fomu za Uteuzi kwa wagombea wa Ubunge na Udiwani ni tarehe 12/08/2020 mpaka 25/08/2020 ambapo Uteuzi kwa Wagombea wote ni tarehe hiyo hiyo ya kurudisha Fomu 25/08/2020.

Zaidi ya hayo, Mwenyekiti alieleza kuwa Kampeni zitaanza tarehe 26/08/2020 na kumalizika tarehe 27/10/2020 na kwa Tanzania Zanzibar kampeni zitamalizika tarehe 26/10/2020 ila siku ya Uchaguzi kwa pamoja siku ya Jumatano tarehe 28/10/2020.

No comments: