Makamu wa Rais apongeza Shilingi milioni 200 za CRDB Bank Marathon kusaidia watoto

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (katikati) akipokea mfano wa hundi yenye thamaani ya sh. milioni 200 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) na kuikabidhi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi (kulia), katika kilele cha mbio za hisani zilizoandaliwa na Benki ya CRDB (CRDB Marathon 2020), jijini Dar es salaam leo. Benki ya CRDB iliandaa mbio hizo kwa lengo la kuchangisha fedha za kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto waliopo kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Muhimbili jijini Dar es salaam.

=====   =====   =====

Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amewapongeza watanzania kwa kukubali na kushiriki kuchangia zaidi ya Sh. Milioni 200 kupitia mbio za hisani zilizoandaliwa na Benki ya CRDB “CRDB Bank Marathon” zitakazofanikisha upasuaji wa moyo kwa watoto 100 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mbio hizo za hisani zilizobeba kaulimbiu isemayo ‘Kasi isambazayo Tabasamu’ ziliizoanzia na kuishia kwenye viwanja vya The Greens Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Mama Samia Suluhu amesema Serikali inafurahishwa na jitihada zinazofanywa na benki hiyo katika kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili jamii kama ilivyo kwa watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa ameambatana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiwa katika Matembezi ya Kilomita 5 kwa ajili ya kuchangia gharama za upasuaji wa Moyo kwa Watoto katika Taasisi ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam leo Agosti 16,2020. Matembezi hayo yameandaliwa na Benki ya CRDB pamoja na mbio za nusu Marathon. kulia kwa Makamu wa Rais ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Abdulmajid Nsekela na kushoto kwa Dkt. Kikwete ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.

“Kwa mda mrefu tumeshuhudia mkiwekeza nguvu katika kusaidia afya ya mama na mtoto, na sasa hivi mmeenda mbele Zaidi kwa kuhusisha wadau wengine katika jitihada hizi, hongereni sana,” alisema Mama Samia Makamu wa rais alisema kwa kiasi kikubwa Serikali imefanikiwa kupunguza changamoto ya kukosa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo hapa nchini kwa kuanzisha Taasisi ya Moyo JKCI.

 “Hii imesaidia kupunguza gharama kwa Serikali ambapo hapo mwanzo tulikuwa tukiwapeleka nje ya nchi,” alisema huku akibainisha kuwa watoto wachache walipa nafasi hiyo kutokana na gharama kuwa kubwa.

Tokea kuanzishwa kwake mwaka 2015, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imefanya upasuaji kwa watoto zaidi ya 1,000. Pamoja na mafanikio hayo wazazi na walezi wengi wenye watoto wenye maggonjwa ya moyo wamekuwa wakishindwa kumudu gharama hizo ambazo sehemu huchangiwa na Serikali.
Sehemu ya Washiriki wa Mbio za 21.1 KM za CRDB Bank Marathon, wakianza kutimka.

‘Niwapongeze wote mlioshiriki kuchangia kusambaza tabasamu kwa watoto hawa na familio, huu ndio uzalendo ambao watoto wetu wanapenda tuuonyeshe kwao,’ aliongezeaMakamu wa Rais huku akiwataka wadau wengine wa Maendeleo kufuata nyayo za Benki ya CRDB.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alielezea ushirikiano uliopo baina ya Benki ya CRDB na Taasisi ya Moyo katika kusaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo na kwamba benki hiyo imekuwa ikitoa  msaada wa gharama za matibabu ambapo mwaka jana benki hiyo ilitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto 50 na mapema mwaka huu ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya watoto 25.

“Kauli mbiu ya mbiu yetu katika mbio hizi za hisani ni ‘Kasi Isambazayo Tabasamu’, ikihamasisha watu ushiriki wa kila mmoja wetu utasaidia kuleta tumaini la maisha na kusambaza tabasamu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa washiriki zaidi ya 4,000 wameweza kushiriki mbio hizo za hisani za mwaka huu.

“Pamoja na jitihada za Serikali kupitia Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Benki yetu ya CRDB bado watoto wengi wamekuwa wakikosa matibabu kutokana na wazazi au walezi kutomudu gharama za upasuaji ambazo ni kati ya Shilingi Milioni 2 hadi Milioni 20,” alisema Nsekela.

Nsekela alizishukuru taasisi za Sanlam, Strategis, Alliance, ARIS, Cool Blue, EFM na TVE na wengineo kwa kujitokeza kushirikiana na Benki ya CRDB kufanikisha CRDB Bank Marathon, huku akiwashukuru maelfu ya watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jitihada za utoaji huduma za upasuaji moyo kwa watoto. Profesa Janabi alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha Watanzania kujisajili kwa wingi kushiriki mbio hizo za hisani ili kusaidia upasuaji kwa watoto.

“Takwimu zinaonyesha watoto milioni 2 wanazaliwa nchini Tanzania wakati asilimia 1 kati yao huwa na magonjwa ya moyo. Ni wajibu wetu sisi kama jamii kuhakikisha watoto hawa wanapata matibabu stahiki, hivyo ushiriki wetu katika mbio hizi za hisani utusaidia kusambaza tabasamu kwa watoto hawa” alisema Profesa Janabi.

Akihitimisha mkutano huo Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea Sera maalum ya kusaidia jamii “Corporate Social Responsibility Policy” ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida ya kutumika katika kusaidia jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira, ambapo mwaka jana pekee Benki ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 1.2.

“Uanzishwaji wa mbio za hisani za CRDB Bank Marathon utasaidia kuongeza ushiriki wa wadau wengi zaidi katika Maendeleo katika sekta hizi za afya, elimu na mazingira,” alisema Nsekela.

Naye Waziri wa Michezo, Dkt. Harison Mwakyembe aliipongeza Benki ya CRDB kwa kutumia michezo kuhamasisha watanzania kushiriki katika shughuli za kijamii. “Nimefurahi mmekuja na ubunifu huu wa kkutumia mbio za hisani kupanua ushiriki wa watanzania katika kutatua changamoto zinazotukabili, ama kweli hii ni Benki inayoongoza kwa ubunifu,” alisema Dkt. Mwakyembe.

“.. mmesema ni kasi isambazayo tabasamu, na kweli tumeona kwanza kwenye kukimbia ambapo tumeboresha afya zetu hasa afya ya moyo lakini vilevile tumewasaidia watoto wenye uhitaji na kwa hilo tumeweka hazina njema kwa Mungu,” aliongezea Dkt. Mwakyembe. Viongozi mbalimbali wa taasisi na serikali walihudhuria mbio hizo za hisani ikiwamo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na mama Salma Kikwete.










No comments: