MAAFISA MAENDELEO WATAKIWA KUSAIDIA KUWAPATA WABUNIFU NA KUVUMBUA VIPAJI KWENYE MAENEO YAO
Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii Mikoa na Wathibiti Ubora wa Shule nchini kusaidia kuwapata wabunifu na kuvumbua vipaji kwenye maeneo yao ili viweze kuendelezwa.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa maafisa maendeleo hao wa mikoa na wathibiti ubora wa shule.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Prof Mdoe amesema vipo vipaji vingi nchini na wataalamu mbalimbali wa teknolojia na wenye Ubunifu hivyo kuwataka maafisa hao kuhakikisha wanaviibua vipaji hivyo ili serikali iweze kuvisaidia kukua zaidi na kufikia malengo yao.
Amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli imenyanyua na kuibua vipaji vya watanzania wa kada mbalimbali kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Prof Mdoe amesema mathalani kwa mwaka 2020/21 serikali ilitenga Sh Milioni 874 kwa ajili ya kazi hiyo ya kuwaendeleza wabunifu hao ili wainue vipato vyao lakini pia kuwa msaada kwa Taifa katika kuinua uchumi hasa wa viwanda.
" Niwaombe ndugu zangu mafunzo haya mtakayoyapata leo yakawe mwanzo kwenu katika kuviibua vipaji vilivyopo kwenye maeneo yenu ili tuweze kuwainua na kuwaendeleza.
Kupitia mafunzo haya sasa tunaamini maafisa maendeleo na wathibiti ubora watakua daraja baina ya serikali kwa maana ya Wizara na wabunifu wetu kwenye maeneo yenu." Amesema Prof Mdoe.
Amesema Wizara ina jukumu kubwa la kukuza vipaji na Ubunifu na kuendeleza watalaamu wa ndani na kuhamasisha Ubunifu na teknolojia mbalimbali ili kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Prof Maulilio Kipanyula amemshukuru Prof Mdoe kwa kukubali wito wao wa kwenda kufungua mafunzo hayo ambayo anaamini yatachochea kuvumbua wabunifu na wataalamu wa teknolojia kwenye mikoa.
Prof Kipanyula amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa ufahamu kuhusu teknolojia na ubunifu ambapo kupitia mafunzo hayo wana uhakika wa kuongeza idadi kubwa ya watanzania wenye uelewa wa teknolojia na ubunifu.
Mafunzo hayo yanahusisha maafisa maendeleo na wathibiti ubora wa shule wapatao 52 kutoka kila Mkoa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja kwa maafisa maendeleo wa mikoa na wathibiti ubora wa shule jijini Dodoma leo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa maendeleo na wathibiti ubora wa shule kwenye uzinduzi wa mafunzo jijini Dodoma.
Maafisa Maendeleo na Wathibiti Ubora wa Shule mbalimbali wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe wakati wa uzinduzi wa mafunzo yaliyoandaliwa na wizara leo jijini Dodoma.
No comments: