HUKUMU KESI ZA UCHAGUZI ZIANDIKWE KWA LUGHA NYEPESI: JAJI MKUU


Majaji wakiwa kwenye mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi yaliyoanza leo jijini Dodoma.

……………………………………………………………….
Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji na
Mahakimu watakaosikiliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu kuandika hukumu hizo katika
lugha nyepesi, inayoeleweka na inayoelimisha wananchi.

Akifungua mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa
Maafisa 282 wa Mahakama wakiwemo waheshimiwa Majaji leo jijini Dodoma,
Jaji Mkuu pia amewataka Wasajili kujitayarisha kutoa muhtasari wa hukumu
husika kwa lugha nyepesi kila hukumu inaposomwa baada ya shauri la uchaguzi
kukamilika ili wananchi waweze kujifunza.

“Katika mafunzo haya, kutakuwa na muwezeshaji atakayewaongoza katika
uandishi wa hukumu katika mashauri ya uchaguzi (Judgment Writing for Election
Petitions and Related Cases), hivyo tumieni wakati huu kujifunza uandishi wa
mihutasari yenye kubeba mafunzo kwa wananchi bila kutumia maneno ya kisheria
na kiufundi”, alisema.

Alisema Mahakama, inatakiwa kutenda haki, hivyo mafunzo hayo ni sehemu ya
matayarisho yatakayowezesha kutimiza wajibu huo wa kutoa haki katika masuala
ya Uchaguzi. Aliongeza kuwa Ibara ya 113 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, inawakumbusha Majaji, Mahakimu na Wasajili kutojiunga na chama
chochote cha siasa, isipokuwa wanayo haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara
ya 5 ya Katiba.

“Katazo hili linatambua wajibu wetu Majaji, Wasajili na Mahakimu ili Mahakama
isionekane kupendelea au kukandamiza upande wowote unaoshindana katika siasa
na katika uchaguzi mkuu, lengo likiwa ni kuwatayarisha Majaji na Mahakimu
kusikiliza mashauri ya uchaguzi kwa weledi, kwa wakati na kwa uwazi na haki”,
alisema Jaji Mkuu.

Amewataka Majaji na Mahakimu kuamua mashauri ya uchaguzi kwa uwazi,
utulivu, kujiamini na kuamini kile wanachokifanya kwa mujibu wa sheria na

utaratibu ili kuongeza imani ya wananchi kwa Jaji au Hakimu husika na kwa
Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.

Alisema nafasi ya Mahakama katika kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwapa
watanzania Uchaguzi huru na wa haki, usio na vitendo vya jinai ni kwa Mahakama
kutimiza wajibu wake wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi katika mashauri
ya jinai yatakayojitokeza katika hatua mbali mbali za uchaguzi kwa haraka na
kuacha Kuahirisha kusiko na lazima.

Jaji Mkuu alisema kufunguliwa kwa mashauri ya kupinga matokeo ya uchaguzi
mahakamani isichukuliwe kuwa ni kuonyesha udhaifu bali mashauri hayo
yachukuliwe kuwa ni nafasi kwa wananchi kuhakikishiwa kuwa uchaguzi
uliomalizika ulikuwa huru na wa haki kama Katiba ya Tanzania inavyotaka.

Alifafanua kuwa Katiba inampa Mwananchi haki ya kupiga kura, kugombea nafasi
ya uongozi na pia inampa haki ya kufungua shauri mahakamani. “Haki ya kupiga
kura na kupigiwa kura hazitakuwa maana endapo hazitaambatana na haki ya
kufungua shauri la uchaguzi pale mgombea anapoamini kuwa uchaguzi haukuwa
huru na wa haki’, alisema.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanalenga kuwajengea uwezo
maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi
Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Awamu ya kwanza ya mafunzo yaliyoanza leo katika ukumbi wa mikutano wa
Takwimu-Dodoma yanawahusisha Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu,
Wasajili na Naibu Wasajili, na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za
Hakimu Mkazi.

Aidha, awamu ya pili itawajumuisha waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya
Rufani na yatafanyika Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu Wakazi
Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye
katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto-Tanga.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu wasajili, Mahakimu pamoja na

wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya
Kurekebisha Sheria ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.

No comments: