ASHIKILIWA NA TAKUKURU MANYARA KWA KUZUIA FEDHA KWA MIAKA 10

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, inamshikilia mkazi wa Mjini Babati Yuda Sendeu akidaiwa kuzuia shilingi milioni 44.7 fedha za chama cha kuweka na kukopa cha Babati Saccos. 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati amesema Sendeu alichukua mkopo wa shilingi milioni 35 na kutakiwa kurejesha shilingi milioni 44.7.

Makungu amesema Sendeu alichukua mkopo huo mwaka 2010 na alitakiwa kurudisha mkopo huo baada ya miezi 24 pamoja na riba. 

Amesema uchunguzi unaonyesha Sendeu alifanya makubaliano ya kihalifu na baadhi ya wanachama wa Babati Saccos waliochukua fedha katika Saccos hiyo bila kurejesha. 

Amesema walifanya hivyo ili haki za wanachama waaminifu wa Saccos hiyo ziweze kupotea. 

"Hadi wanachama waaminifu wa Saccos hiyo wanafikisha malalamiko ya dhuluma hiyo TAKUKURU Sendeu, bila kustahili amekaa na fedha hizo kwa miaka 10," amesema Makungu. 

Ametoa rai kwa wanachama wa Babati Saccos wanaofahamu kuwa wamechukua fedha za Saccos hiyo na muda wa kurejesha umepita wafike kwa hiyari kwenye ofisi za TAKUKURU.

Amesema wanatakiwa wafike kwenye ofisi hizo Agosti 10 mwaka huu ili wapewe hesabu zao na kuzirejesha na kwa wale watakaokaidi hatua kali dhidi yao zitachukuliwa kuanzia Agosti 12 mwaka huu. 
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na wandishi wa habari mjini Babati.
 

No comments: