ARUSHA KUMENOGA, MAANDALIZI YA MAPOKEZI YA TRENI YA MAJARIBIO YA ABIRIA YAPAMBA MOTO

Shirika la reli Tanzania linatarajia kufanya safari ya majaribio ya treni ya abiria kutoka Dar es salaam hadi Arusha ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufufua reli ya kaskazini.

Safari hii ya treni ya majaribio ya abiria ni baada ya kupokelewa kwa treni ya mizigo ya majaribio majuma kadhaa yaliyopita.

Maafisa wa shirika la reli Tanzania TRC wakiongozwa na mkurugenzi mkuu Ndg.Masanja Kungu Kadogosa, tayari wako jijini Arusha kwaajili ya maandalizi ya sherehe za mapokezi ya Treni hiyo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Idd Kimanta.

“Maandalizi ya kupokea treni hii ya majaribio yanaendelea vizuri,kwahiyo wananchi wa Arusha nawaombeni sana tufike steaheni ya treni kuipokea treni hii” alisema Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. Idd Kimanta.

Mh. Kimanta aliongeza kuwa Treni hiyo ya majaribio ya abiria itasimama kwa muda katika stesheni ya Usa River na wakazi wa Arusha kupata nafasi ya kuipanda mpaka Stesheni ya Arusha mjini.

Aidha katika mahojiano maalum na Kituo cha Redio cha Sunrise cha jijini hapo,mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Kenani Kihongosi ameipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya tano chini Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa juhudi za kuifufua reli ya kaskazini, hatua ambayo inakwenda kuleta unafuu wa huduma za usafiri na kuchochea maendeleo.

Naye mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk amewataka wakazi wa Mkoa wa Arusha na Kanda ya kaskazini kwa ujumla kuwa walinzi wa miundombinu ya reli ili kuitunza reli kwa maendeleo ya taifa

Safari za Treni kati ya Dar es salaam na Arusha zilisimama kwa zaidi ya miaka 30 kabla ya mpango wa serikali ya awamu ya Tano ya kuifufua njia ya reli ya kaskazini,hatua ambayo inaweka historia mpya kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha na kanda ya Kaskazini.


Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndg. Masanja Kungu Kadogosa (kulia) akimwelezea jambo Mkuu wa mkoa wa Arusha Mh. Idd Kimanta,alipomtembelea nyumbani kwake jijini humo ikiwa ni kuelekea mapokezi ya treni ya abiria ya majaribio kutoka Dar es salaam -Arusha tarehe 24 Agosti 2020
 Mkuu wa wilaya ya Arusha Mh.Kenani Kihongosi akifafanua jambo wakati wa mahojiano maalum na kituo cha redio cha Sunrise cha jijini Arusha,juu ya mapokezi ya Treni ya abiria ya majaribio kutoka Dar es salaam - Arusha,Kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu na utawala TRC, Amina Lumuli  na kulia ni mkuu wa kitengo cha Habari na Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk.

No comments: