WAZIRI MKUU: NI WAJIBU WETU WATANZANIA KUENDELEA KUMUOMBEA HAYATI RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwenye geneza lenye mwili wa mpendwa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kwenye uwanja wa Uwanja wa Uhuru  jijini Dar es Salaam leo.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema leo Julai 28,2020 tumekutana Uwanja wa Uhuru kuaga kitaifa kutokana na kifo cha baba yetu, mpendwa wetu na Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, hivyo ametumia nafasi hiyo kuendelea kumpa pole Rais Dk.John Magufuli.

Ametumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania wote kuendelea kuyaenzi yale yote mazuri ambayo yalifanywa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa katika utumishi wake kwa Taifa la Tanzania na jukumu lililopo mbele yetu ni kuendelea kumuombea kwa Mungu.

Akizungumza leo asubuhi wakati akifungua rasmi shughuli za kuaga mwili mzee wetu Mkapa kitaifa, Waziri Kassim Majaliwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi Taifa amesema anaipongeza kamati hiyo kwa kufanikisha tukio hilo la kuaga kitaifa."Nawashukuru watanzania kwa kujitokeza kwa wingi kumuaga mpendwa wetu.

"Kwa siku ambazo zilitolewa kwa ajili ya kuaga watanzania wamejitokeza kwa wingi na tulitoa siku mbili kwa ajili ya kutoa nafasi ya wananchi kuaga na wale ambao hawakupata nafasi ya kufika nao watakuwa wameshiriki kwa namna moja au nyingine."

"Mataifa mbalimbali nayo yameguswa na tukio hilo na wameungana nasi katika siku hii ya kuaga kitaifa.Jambo hili halivumiliki, halitasahaulika.

Mzee wetu amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya nchi yetu, watanzania wametoa hisia zao, wajibu wetu sasa ni kumuombea, kuenzi yote mazuri ambayo tunayafahamu na kuyasema, najua wote tuna uchungu, tunahuzuni lakini tuendelee kumuombea."Amesema Waziri Mkuu.

Kuhusu shughuli ya leo amesema haitakuwa ndefu sana kwani itakuwa ni siku ya kuaga kwa viongozi wakuu kwa kuanza na mkewe wa hayati Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa akiambatana na Rais Dk.John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, marais wastaafu pamona na viongozi wengine kulingana ana utaratibu uliowekwa.

No comments: