WADAU WAHAMASISHWA KUIMARISHA USAFI SHULENI


Na Mwandishi wetu, Dodoma

Wadau na mashirika mbalimbali wamehimizwa kuchangia vifaa vya kuimarisha usafi kwenye shule za msingi na sekondari ili kuwakinga watoto na maradhi ikiwemo Covid 19.

Akipokea vifaa vya kisasa vya kunawia kutoka shirika la Compassion na kuvikabidhi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya shule 22, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya watoto kutoka Wizara ya Afya Mwajuma Magwiza, amesema wadau wengine bado wanahamasishwa ili waweze kuimarisha mazingira yote ya kujifunzia ikiwemo mazingira ya usafi na vyoo.

"Lengo siyo kujikinga na ugonjwa wa Corona tu ambao bado tunapambana nao, lakini ni kujenga tabia ya usafi kwa watoto wetu wakiwa shuleni" alisema.

Magwiza ameongeza kuwa, wadau wanaofanya kazi za kuhakikisha utoaji wa haki kwa watoto, wanahamasishwa kuimarisha na kujenga mazingira wezeshi ya watoto kujifunzia na kuwalinda dhidi ya maradhi na changamoto mbalimbali.

"Bado tunawahamasisha wadau, mazingira haya ya kujenga miundombinu mizuri shuleni siyo tu kwenye vifaa vya kunawia, lakini pia vyoo na maji bado ni changamoto hasa shule za pembezoni" alisisitiza Magwiza.

Amewataka Walimu wa shule hizo zilizopata vifaa vya kunawia kuhakikisha wanavitunza ili visaidie kuboresha hali ya usafi katika Shule hizo.

Naye Afisa  Elimu Sekondari wa jiji la Dodoma Fardinand Komba, akipokea vifaa hivyo amesema vifaa hivyo vimefika kwa muda muafaka, kwani shule zilizopata vifaa hivyo ziko pembezoni mwa Dodoma jiji ambako si rahisi kuvipata. Aidha Ameishukuru Wizara pamoja na wafadhili kwa kuwezesha Jiji la Dodoma kupata vifaa hivyo.

"Serikali wakati inatoa maelekezo wakati wa kufungua shule kuwepo kwa vifaa hivi kila shule, kwa msaada huu mmetoa nafasi zaidi kwa wanafunzi wengi kusafisha mikono yao bila matatizo yoyote" amesema.

Ameongeza pia tabia ya kunawa mikono imepunguza mambo mengi na kuwa tangu shule zifunguliwe hakuna taarifa ya mtoto kupata ugonjwa wa Covid 19 aidha, magonjwa ya kuharisha yamepungua.

Mwakilishi kutoka Shirika la Compassion Melkzedek Carol amesema wanaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano mkubwa wanaopata katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama.

" Kwa nchi nzima shirika la Compassion kwa kushirikiana na Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii limetumia jumla ya sh. Bilioni 1.2 kuhakikisha watoto wanakuwa salama dhidi ya magonjwa hasa wakati wa janga la Corona" amesema Carol.

Naye mmoja wa walimu wakuu waliopokea vifaa vya kunawia Salome Mkombola ameshukuru Serikali na wafadhili kwa msaada huo na kuahidi kutumia vizuri vifaa hivyo, huku akiomba na shule nyingine zipate pia.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watoto wa Wizara ya Afya Mwajuma Magwiza akiangalia vifaa vya kunawia mikono kabla hajavipokea na kuvikabidhi kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka Shirika la Compassion kwa ajili ya shule 22 za Jijini hapa.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watoto wa Wizara ya Afya, Mwajuma Magwiza akimkabidhi vifaa vya kunawia mikono kwa mwakilishi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa Dodoma kwa ajili ya shule 22 jijini hapo baada ya kuvipokea kutoka shirika la Compassion.
Mhandisi Nyangusi Matalani ( kushoto) akielekeza jinsi ya kutumia vifaa vya kunawia mikono kwa ajili ya shule 22 za Jiji la Dodoma wakati wa makabidhiano yaliyofanyika kati ya Wizara ya Afya na shirika la Compassion.Picha zote na WAMJW

No comments: