LISSU ASHINDWA KUFIKA MAHAKAMANI KISAKUJIWEKA KARANTINI
Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa mshtakiwa Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi ameshindwa kufika mahakamani leo kwa kuwa ameamua kujiweka karantini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu.
Aidha mahakama hiyo pia imetoa hati ya wito kwa mshtakiwa Lissu ikimtaka afike mahakamani hapo Agosti 26, 2020 bila kukosa.
Mapema kesi za uchochezi namba 123 ya mwaka 2017 na kesi namba 236 ya 2017 dhidi ya Lissu ziliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa
Akitetewa na wakili Peter Kibatala katika kesi ya uchochezi namba 123 ambayo Lissu amejidhamini mwenyewe imedaiwa, mshtakiwa ameshindwa kufika mahakamani leo kwa kuwa ameshauriwa kujiweka karantini kufuatia kuishi nje ya nchi kwa muda mrefu alipokuwa anapatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
" Mheshimiwa, mshtakiwa alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu, na amerudi jumatano, katika kipindi hicho alikuwa akikutana na watu wengi hivyo amshauriwa akawe isolation (karantani) kwa siku 14 ili kupunguza risk ya kuambukiza magonjwa na tarehe itakayopangwa atakuwepo kutekeleza amri za mahakama" amesema Lissu.
Upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa serikali Mkuu Renatus Mkude akisaidian na wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon umedai kuwa hawana pingamizi na Hakimu mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 26, mwaka huu.
Katika kesi namba 236, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili hao wamedai kesi hiyo leo imekuja kwa ajili ya kutajwa Lakini mshtakiwa Lissu na wadhamini wake wote hawajafika hivyo wameomba mahakama itoe hati ya wito ya kumuita mshtakiwa huyo.
Hata hivyo wakili Kibatala aliomba msamaha kwa ajili ya wadhamini akidai yeye ndio alikosea kuwapa taarifa wadhamini kwa kuwaeleza kuwa kesi ni Jumatatu kumbe ni leo Julai 30,2020 ila amedai mshtakiwa siku atafika mahakamani bila kukosa.
Katika kesi namba 123, Lissu anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Deman, Zanzibar, Januari 11, 2017, akiwa eneo la Kibunju Maungani, Wilaya ya Magharibi B, mkoni Mjini Magharibi.
Lisu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari 9,2017 na kusomewa mashtaka matano ya uchochezi, kutokana na maneno aliyoyasema siku hiyo.
Katika kesi namba 236, Lissu anadaiwa kuwa Julai 17, 2017 akiwa eneo la Ufipa, Wilaya ya Kinondoni ndani ya Jiji la Dar es Salaam alitoa maneno ya chuki.
Maneno hayo; "Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.Vibali vya kazi work permit vinavyotolewa kwa wamishenari wa kikatoliki tu huku mashehebu mengine yakielezwa kupanga foleni uhamiaji,
" Viongozi wakuu wa Serikali wanachaguliwa kutoka kwenye familia,kabila na ukanda...Acheni woga pazeni sauti...kila mmoja wetu...tukawaambie wale ambao bado wanampa msaada wa pesa Magufuli na Serikali yake kama tulivyoambiwa wakati wa Serikali ya Makaburu, hii Serikali isusiwe na jumuiya ya kimataifa, isusiwe kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa sababu ya utawala huuwa kibaguzi...yeye ni dikteta uchwara",.
Ilidaiwa kuwa maneno hao yalikuwa yana lengo ya kusababisha chuki.
No comments: