WAZIRI WA FEDHA DK.MPANGO AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA JINSI ANAVYOLIONGOZA VEMA TAIFA, AGUSIA CORONA , MAFURIKO
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango ametoa pongezi za dhati kwa Rais Dk.John Magufuli kwa jinsi alivyoendelea kuliongoza vema Taifa letu huku akifafanua kwa kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wake tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi , mfumuko wa bei umethibitiwa na miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa.
Pia amesema wajibu katika utumishi wa umma umeimarika na kero za wananchi wanyonge zimetatuliwa, hivyo kwa kipekee kumuamini kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango tangu mwanzo wa uongozi wake hadi sasa.
Dk.Mpango ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2020/2021 ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa nchi yetu imepata mvua nyingi zilizo juu ya wastani hali iliyosababisha kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali.
Amesema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima, mali na miundombinu hususan barabara, reli na madaraja.Mafuriko hayo yameathiri utelekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za ukarabati wa miundombinu iliyoharibika. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/21 kipaumbele ni kukarabati miundombinu iliyoharibika.
Pia amesema kama unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla ilikabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama COVID - 19 inayosababishwa na virusi vya Corona. Hivyo ni dhahiri ugonjwa huo umeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani kutokana na vifo, kuongezeka kwa gharama za utoaji huduma katika sekta ya afya na kuathiri shughuli za biashara na uzalishaji hususan kwa nchi zinazotegemea utalii.
"Jambo jema ni kuwa nchi yetu haikuathirika sana na ugonjwa huu kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi imara wa Dkt. John Pombe Magufuli.Kama Taifa tuliendelea kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuchukua tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na wataalam pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
"Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu ambapo hadi sasa Serikali imetoa kiasi cha Sh.bilioni 15.49 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kinga. Hatua nyingine ni pamoja na kutolewa msamaha wa kodi kwa aina 15 za vifaa vya kupambana na COVID – 19; kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi; kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uangalizi kwa wasafiri wanaoingia nchini na wanaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huu.
"Na kuanzishwa kwa huduma ya namba maalum ya kupiga simu bila malipo kwa ajili ya msaada wa kiafya. Vile vile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali za Sera ya Fedha ili kulinda na kuimarisha uchumi zikijumuisha.Pia kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 7 hadi 6,"amesema.
Mengine ambayo yamefanyika ni kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 7 hadi 5, kupunguza kiwango cha dhamana za Serikali kutoka asilimia 10 hadi 5 kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia 40 hadi 20 kwa hati fungani pamoja na kuzielekeza kampuni zinazotoa huduma za fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa mteja kutoka shilingi milioni 3 hadi 5 na kiwango cha akiba kwa siku kwa wateja kutoka shilingi milioni 5 hadi 10.
Amesema kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali, hivi sasa hali imeimarika ambapo shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika kama awali. Serikali imeruhusu vyuo vikuu vimefunguliwa, wanafunzi wa kidato cha sita wamerudi shuleni kujiandaa na mitihani, shughuli za michezo yote zimeruhusiwa.
"Anga limefunguliwa ambapo ndege za mizigo na abiria zinaendelea kuingia nchini na hivyo kupokelewa kwa watalii kutoka nchi mbalimbali. Hii ni ishara dhahiri ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais kwa Taifa hususan katika kipindi cha majanga na misukosuko mikubwa kwa dunia kama ugonjwa huu,"amesema Waziri Mpango .
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, jijini Dodoma.
No comments: