WANA CCM,WANANCHI WAJITAFAKARI KUMCHAGUA KIONGOZI ATAKAYEWAFAA KUWAONGOZA KIPINDI KIJACHO-BALOZI SEIF ALI IDDI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati muda wa kuelekea katika uchaguzi Mkuu unakaribia Wana CCM na Wananchi wana fursa nzuri ya kutafakari Kiongozi atakayefaa kuwaongoza katika kipindi kijacho cha Miaka Mitano.
Alisema Viongozi wanaofaa kushika hatamu ya kuwaongoza vyema ni wale wenye uwezo kamili wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayokwenda kisasa katika mazingira ya Karne ya sasa ya Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduziu Dr. Ali Mohamed Shein katika uzinduzi wa Tangi kubwa la Kuhifadhia Maji safi na salama pamoja na uzinduzi wa Ofisi ya Jimbo la Kikwajuni iliyofanyiwa matengenezo makubwa ikiwa ni umaliziaji wa Utekelzaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo hilo.
Alisema Wananchi wanapaswa kufanya tathmini ya kina itakayoweza kuwaibulia mchapakazi imara atakayejitolea kusimamia kwa wakati wote masuala yao ya Maendeleo na Uchumi katika maeneo yao.
Alibainisha kwamba kumchagua Kiongozi kabla ya kumfanyia uhakiki wa kina huleta hatari kwani matokeo yake ni majuto yasiyokuwa na suluhu na hata kama uchaguzi wenyewe ukiambatana na rushwa inayokuwa kaa la moto ndani ya Miaka Mitano ya yule aliyechaguliwa.
“ Wagombea waliopenya na wale watakaopenya kwenye kampeni kabla ya wakati Chama hakitosita kuwachukulia hatua za nidhamu ikiwemo kuwakata katika mchakato wa kumtafuta mgobmea”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Balozi Seif alisisitiza kwamba Wanachama wa Chama cha Mapinduzi lazima waendelee kuwa na kauli Moja itakayotoa nguvu ya ushindi ili CCM iendelee kushika Dola na kuwahudumia Wananchi wote Tanzania katika kipindi kirefu kijacho.
Alielezea faraja yake kutokana na Utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi kwa Mwaka 2015 - 2020 uliofanywa na Chama cha Mapinduzi Tanzania hasa upande wa Zanzibar kwa vile haukupata vikwazo wala msukosuko kama ilivyokuwa 2010 – 2015 kutokana na wasimamizi wake kuwa na kauli moja katika utekelezaji huo.
Alisema Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali zake zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar bado kina dhima ya kuendelea kulinda Amani na utulivu uliosaidia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa Maendeleo ya kupigiwa mfano ndani ya Bara la Afrika.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwakumbusha Wanachama wenye nia ya kuchukuwa Fomu kwa ajili ya kuomba Uongozi ndani ya CCM wazingatie Sheria, Muongozo na Taratibu zilizowekwa.
Aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Kikwajuni kwa kazi kubwa ya kuwaletea Maendeleo Wananchi wake wakiwemo wale wa Mitaa ya jirani kazi iliyoleta Mafanikio Makubwa na ya kupigiwa mfano ndani ya Utekelezaji wa Ilani ya Chama ikienda sambamba na utekelezaji wa Ahadi uliyotoa wakati wa Kampeni.
Balozi Seif Ali Iddi akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali amewaonya Watu au Kikundi chochote chenye nia ya kutaka kuleta vurugu Nchini hasa kipindi cha kuelekea Kampeni na Uchaguzi wenyewe kwamba Vyombo vya Dola havita sita kuwachukuliwa hatua zinazofaa za Kisheria dhidi yao.
Akigua Virusi vya Corona Balozi Seif amesema maradhi hayo bado yapo. Hivyo ni vyema Kila Mwananchi akaendelea kuchukuwa tahadhari ya Kujikinga ili kuepuka maambukizi Mapya.
Alisema ni vyema ushauri wa Wataalamu wa Afya ukaendelea kuzingatiwa kwa kunawa Mikono kwenye Maji yanayotiririka pamoja na kuvaa Maski hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa Watu kama Sokoni au Kwenye vyombo vya Usafiri.
Wakiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni Mh. Nassor Salum Jazira na Mbunge wa Jimbo hilo Mhandisi Hamad Yussuf Masauni wamesema CCM kwenye uchaguzi ujao haitapata shida kuwanadi Wagombea wake watakaopata fursa ya kuteuliwa kugombea Jimbo hilo.
Walisema hiyo inatokana na Utekelezaji mkubwa wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Jimbo la Kikwajuni Wilaya ya Mjini ambayo imepindukia kwa asilimia 100%.
Mh. Nassor Jazira na Mhandisi Masauni walieleza kwamba uimarishaji wa Sekta ya Maji uliosimamiwa na Uongozi wa Jimbo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} umelea Ukombozi mkubwa kwa Wananchi waliowengi ndani ya Jimbo hilo ambao sasa utabakia kuwa Historia kutokana na kuondoka kwa changamoto ya huduma ya Maji.
Walifahamisha kwamba kazi hiyo nzito iliyopata msukumo kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilikwenda sambamba na uimarishaji wa Sekta ya Elimu, Afya, Michezo pamoja na Mawasiliano ya Bara bara na Magari.
Katika shughuli hiyo Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi Kadi za C.C.M kwa Wanachama 31 Waliohama Vyama tofauti vya Upinzani na kuhamia Chama cha Mapinduzi.
Halkadhalika akakabidhi mchango wa Computer na Printer Zake, Garil Moja ya Jimbo, Basi Moja na Seti za Jazi kwa Chuo cha kuwafundishia Vijana masuala mbali mbali ya Michezo na ushoni.
Mapema Katibu wa Chama cha Mapinduzi Jimbo la Kikwajuni Nd. Farid Abdullah Hamad alisema kwa Niaba ya Wanachama na Wananchi wa Jimbo hilo wanaishukuru Serikali Kuu kwa nguvu kubwa iliyochukuwa ya kuimarisha Miundombinu mingi ya Maendeleo ndani ya Jimbo hilo.
Nd. Farid alisema Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni na maeneo jirani wana haki ya kujivunia kutokana na neema ya Maendeleo hayo ambayo wameiomba Serikali kupitia Taasisi yake kutoa upendeleo wa fursa za Ajira kwa ile Miradi ya Uwekezaji iliyoanzishwa katika Jimbo hilo.
Balozi Seif akikabidhi vyakula na vifaa mbali mbali kwa Vijana wa Jimbo la Kikwajuni wanaojishughulisha na Mafunzo ya masuala ya ufundi.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Muonekano wa Tangi Kubwa la Kuhifadhia Maji safi na salama lenye kuhifadhi Lita Laki 250,000 liliopo Jimbo la Kikwajuni ambalo limezinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Balozi Seif Ali Iddi akizindua Rasmi Jengo la Afisi ya CCM Jimbo la Kikwajuni baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa yaliyogharimu Zaidi ya Shilingi Milioni 120,000,000/-.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Wana Chama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi wa Jimbo la Kikwajuni baada ya kuzindua rasmi Tangi kubwa la kuhifadhia Maji Safi na salama pamoja na Ofisi ya Jimbo hilo iliyofanyiwa matengenezo makubwa.
No comments: