VIONGOZI NA WAFUASI 27 WA CHADEMA KUKAMATWA

Na Karama Kenyunko Michuzi TV 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa hati ya kukamatwa kwa wafuasi watano wa Chadema  wanaokabiliwa na kesi ya jinai yenye mashitaka saba mahakamani hapo  baada ya kukiuka masharti ya dhamana.

Katika kesi hiyo, viongozi na wafuasi 27 wa Chadema wanakabiliwa na mashtaka saba likiwemo la kukaidi amri halali na kuharibu geti la gereza la Segerea.

Washitakiwa hao ambao  hawajafika na kuamriwa kukamatwa ni Edga Adelin, Gerva Yenda, Regnald Masawe, Cesilia Michaeli na Paulo Makali.

Mapema, wakili wa Serikali Ester Martin alidai mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi,kuwa kesi hiyo leo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali lakini upande wa mashtaka haujajiandaa hata hivyo washtakiwa wengine hawapo.

Kufuatia m111¹qaelezo hayo Hakimu Shahidi aliuliza kama wadhamini wa washtakiwa wapo ili kueleza sababu za washtakiwa hao kutokufika Mahakamani hata hivyo hakuna mdhamini aliekuwepo.

Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu kwa ajli ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washitakiwa wengine  katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa baraza la wananwake (bawacha) Halima Mdee, aliyekuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani Ester Bulaya,  Mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida Jesca Kishoa, aliyekuwa Meya wa Ubungo Boniface Jacob, Diwani wa Tabata Patrick Assenga na Mshewa Karua.

Wengine ni  Khadija Mwago, Pendo Mwasomola, , Happy Abdallah, Stephen Kitomali,Athumani Hassan, Omary Milodo, Emmanuel Ignastemu, Stephen Kitomali, Hamis Yusuph, Juma Juma, Mustafa Lada, Emmanuel Zakaria na Steven Ezekiel.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Machi 13, 2020 washitakiwa hao wakiwa katika gereza la Segerea lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, isivyo halali na kwa makusudi walikaidi amri iliyotolewa na askari B 3648 SGT John ambaye  aliwataka wahusika hao kuondoka eneo hilo la magereza na alikuwa akitimiza wajibu wake aliyopewa.

Mashtaka mengine ni kukusanyika eneo la Magereza isivyo halali na kupelekea kuleta hofu na kuhatarisha amani na utulivu kwenye eneo hilo,kufanya uharibifu wa geti la Segerea ambalo ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mashtaka mengine ni kutoa lugha ya kuudhi ambalo linalomkabili Mdee na Bulaya ambapo inadaiwa siku hiyo walitoa maneno ya kuudhi kwa askari magereza Sajenti B 3648 John, maneno ambayo yalipelekea uvunjifu wa amani.

Pia inadaiwa katika tarehe hiyo mshitakiwa Jacob akiwa eneo la gereza la Segerea alitamka maneno ya kuudhi kwa Sajenti B 3648 John na kufanya shambulio kwa askari magereza huyo kwa kumkunja na kumvuta shati wakati akitekeleza majukumu yake.

No comments: