UWT DODOMA MJINI YAMUUNGA MKONO RAIS MAGUFULI KWENYE SEKTA YA AFYA NA ELIMU
Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuunga mkono juhudi za Rais Dk John Magufuli za kuwahudumia watanzania, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Dodoma Mjini umekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh Milioni Mbili kwenye sekta ya Afya na Elimu wilayani humo.
Vifaa vilivyotolewa na UWT Wilaya ya Dodoma Mjini ni Mashuka 50 ya kujifunikia katika Kituo cha Afya Mkonze ambacho kilikua kinatumika kuhudumia wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa wa Corona na vifaa vya kufanyia mitihani katika Shule ya Sekondari Wasichana Msalato.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Katibu wa UWT Wilaya hiyo, Diana Madukwa amesema juhudi kubwa za kimaendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli ndizo ambazo zimewafanya waone kwamba nao wanapaswa kumuunga mkono kwa kuchangia vifaa hivyo.
Amesema pia wametoa vifaa hivyo kama pongezi pia kwa Rais Magufuli kwa uwezo wake mkubwa alioonesha katika mapambano dhidi ya Corona ambapo kwa kiasi kikubwa maambuzki yamepungua na shughuli za kimaendeleo zinaendelea kama kawaida.
" Tumeguswa sana na kazi kubwa anayofanya Rais wetu Dk John Magufuli, amejenga vituo vingi vya afya nchi nzima, sisi Dodoma tuna vituo vya afya vikubwa tena vyenye hadhi ya Hospitali kabisa, haya mashuka tuliyoleta hapa Mkonze ni kuonesha jinsi gani tunamuunga mkono.
Hiki Kituo kilitumika kuhudumia wagonjwa wa Corona na hakika walifanya kazi kubwa sana, tunaamini idadi hii ya mashuka tuliyoleta itakua msaada na mchango mkubwa kwa wananchi wanaokuja kutibiwa na kulazwa hapa," Amesema Madukwa.
Amesema wao kama UWT Wilaya ya Dodoma Mjini wameona wasibaki nyuma kwani licha ya serikali kujenga wodi za wagonjwa na nyumba za watoa huduma wao kama Chama chenye ilani wana wajibu wa kuunga mkono mazuri yanayofanywa na serikali.
"Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM na sisi tumejionea utekelezaji mzuri wa ilani yetu, tukasema kama Wanawake wa Dodoma Mjini hebu tuje pia kuweka mchango wetu wa mashuka 50," Amesema Madukwa.
Amewapongeza watoa huduma wa Kituo hiko kwa moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kuwahudumia wagonjwa wote wa Corona waliokua wanaletwa kituoni hapo hadi wakati huu ambao hakuna hata mgonjwa mmoja alielazwa na waliokuepo wakiwa wamepona na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao.
Umoja huo pia ulitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato kujionea maandalizi yao ya mitihani ya kidato cha sita ambapo walikabidhi vifaa mbalimbali vya kufanyia mitihani kwa wanafunzi wote 60.
Madukwa amesema vifaa walivyopeleka ni Kalamu boksi 20, Rula 60, Mkebe (Mathematical Sets) 214 na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kuweza kutimiza ndoto zao.
" Kwanza nimpongeze Rais Magufuli kwa kuruhusu shughuli ziendelee ikiwa ni pamoja na kuwaruhusu nyinyi kidato cha sita kurejea shule na kumalizia mitihani yenu licha yakupitia changamoto za Corona.
Hivyo sisi tumekuja kuwatia moyo na kuwapa vifaa hivi ambavyo tunaamini vitakua msaada kwenu lakini na kuunga mkono juhudi kubwa za serikali yetu katika kuboresha elimu nchini, niwaombe mkafanye vizuri kwenye mitihani yenu kwani Taifa linawategemea," Amesema Madukwa.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze, Dk Twilumba Lihweuli ameishukuru UWT Dodoma Mjini kwa kuwapatia mashuka hayo na kuahidi kuwa yatatumika kama ilivyokusudiwa.
" Niwashukuru sana UWT wilayani kwetu, mmeonesha kwa vitendo kuwa mnaunga juhudi za Rais wetu kwenye maboresho anayoyafanya katika sekta yetu ya Afya, huu ni uzalendo mkubwa na sisi tunaahidi kuendelea kuwahudia watanzania na vifaa hivi vitawafikia walengwa, " Amesema Dk Twilumba.
Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari Msalato amesema vifaa hivyo walivyoletewa vitakua chachu kwao katika kufanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita na kuahidi kuwa wanafunzi wote watafaulu kwa kupata daraja la kwanza.
Uongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Dodoma Mjini wakikabidhi mashuka kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Katibu wa UWT Dodoma Mjini, Diana Madukwa na wa kwanza kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Kituo hiko, Dk Twilumba Lihweuli.
Katibu wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa akiwaonesha wanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Msalato Mkebe ambao Umoja huo umewapelekea kwa ajili ya kufanyia mitihani yao inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Mmoja wa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msalato akipokea zawadi ya vifaa vya kufanyia mitihani kutoka kwa viongozi wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini.
Muonekano wa Kituo cha Afya Mkonze ambacho kilikua kinatumika kuwahudumia wagonjwa waliokua wameambukizwa na ugonjwa wa Corona.
Wanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato wakimsikiliza Katibu wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini alipokua akizakizungumza nao.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mkonze, Dk Twilumba Lihweuli akitoa shukrani zake kwa viongozi wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini ambao wametoa mashuka 50 kwenye Kituo hiko.
No comments: