TAKUKURU MANYARA YAMPANDISHA MAHAKAMANI MMILIKI WA KITUO CHA MAFUTA CHA SIMON LEMEYA KWA TUHUMA ZA UHUJUMU UCHUMI

Charles James, Michuzi TV.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro, Manyara kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka itamfikisha katika Mahakama ya Wilaya mmiliki wa Kituo cha mafuta cha Simon Lemeya kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Lemeya atafikishwa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro leo Juni 22 kwa makosa ya kughushi, matumizi ya nyaraka, kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh Milioni 5,609,000 kinyume cha sheria ya uhujumi uchumi Cap 200 marejeo ya 2002.

Taarifa iliyotolewa leo Juni 22,2020 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Makungu imesema uchunguzi wao umebaini kwamba watuhumiwa mnamo mwaka 2014 walighushi nyaraka na kufanya ubadhirifu wa fedha za chanjo ya kitaifa ya Rubella na Surua hivyo kuisababishia hasara serikali.

Uchunguzi unaonesha Ezekiel Mayumba aliandaa fomu za kutokea mafuta ambapo kwa kushirikiana na Simon Lemeya na Simaloy Baby Lemeya mfanyakazi wa Kituo hiko pamoja na Ally Sadick wa kituo cha Membi Filling Station walighushi saini za madereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na kuwezesha kujipatia kiasi hicho cha fedha.

" Kibali cha mashtaka kutoka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP kinachoruhusu watuhumiwa kufikishwa mahakamani kimetolewa, makosa yanayoshtakiwa nayo ni matumizi ya nyaraka kudanganya mwajiri na ubadhilifu chini ya vifungu 22 na 28 vya sheria ya TAKUKURU.

Makosa mengine katika kibali hicho ni yale ya kughushi na kuisababishia hasara serikali ya Sh Milioni Tano kinyume cha aya ya 10(I) jedwali la kwanza na vifungu vya 57(I) na 60(2) sheria ya uhujumu uchumi cap 200 kama ilivyofanyiwa marejeo 2002," Amesema Makungu.

Amesema TAKUKURU Manyara inazo taarifa kwamba washtakiwa wengi wa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi mkoani humo bado wanaendelea na utumishi wa umma licha ya kuwa tayari wana kesi katika mahakama za wilaya na Mkoa wa Manyara.

" Kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 zinawapa mamlaka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kuwasimamisha kazi watumishi wenye mashauri ya jinai mahakamani.

Nitoe rai kwa Wakurugenzi mkoani Manyara kutekeleza wajibu wao wa kisheria punde watumishi wanapofikishwa mahakamani ili kurejesha nidhamu kwenye utumishi wa umma," amesema Makungu.

No comments: