SIKU YA WAJANE DUNIANI, ZAIDI YA WAJANE MILIONI 250 WANAISHI KATIKA DIMBWI LA UMASIKINI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wajane katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Aprili nne, 2019.

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
KUPOTEZA wenza ni jambo linalovunja mioyo ya wanawake wengi duniani hasa kwa nchi zinazoendelea, wajane katika nchi hizo wamekuwa na muendelezo wa kutafuta mahitaji yao muhimu, haki zao pamoja na utu ambapo katika baadhi ya tamaduni nyingi za kiafrika huwachukulia wajane kwa namna ya tofauti ikiwemo kurithiwa na ndugu wa mume na hata kutokuwa na nafasi ya kumiliki au kusema juu ya urithi ulioachwa na waume zao.

Kufuatia changamoto wanazopitia wajane, Umoja wa Mataifa ukatenga siku ya tarehe 23, Juni kila mwaka kuwa siku ya wajane duniani katika maazimio ya A/RES/65/189) tangu mwaka 2011, huku ikishauriwa kutumia siku hiyo kupaza sauti pamoja na kueleza uzoefu kwa wajane ili kushirikiana na kupaza sauti katika kusimamia haki zao.

Licha ya tafiti kuonesha kuwa kuna zaidi ya wajane milioni 250 mlipuko wa virusi vya Corona bado umeacha maelfu ya wajane kwa wakati mmoja huku shughuli zao za kijamii  na kiuchumi zikisimama kutokana na mlipuko huo jambo ambalo zimeendelea kuzipeleka familia nyingi katika janga la umaskini.

Tafiti zinaonesha kuwa mlipuko ya magonjwa yaliyotokea awali ikiwemo UKIMWI  na Ebola wajane wengi walikumbana na changamoto za kurithiwa, kunyang'anywa mali baada ya waume zao kufariki, unyanyasaji (wengi waliitwa waathirika wa magonjwa hayo.)
Inakadiriwa kuwa Kuna zaidi ya wajane milioni 258 duniani kote na wengi wao wanaishi katika dimbwi la umaskini, huku idadi hiyo ikielezwa inaweza kuongezeka zaidi kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona ambao umeathiri dunia nzima.

Matatizo yanayowakumba wajane hasa katika nchi zinazoendelea ni pamoja na umaskini, unyanyasaji pamoja na migogoro ya urithi.

Imeshauriwa kuwa siku hiyo itumike kama fursa kwa vitendo kwa wajane kwa kupaza sauti katika upatikanaji wa haki zao za msingi ikiwemo taarifa za msingi kuhusiana na urithi masuala ya ardhi, umiliki wa rasilimali, mafao pamoja na ulinzi katika jamii.

Aidha imeshauriwa pia katika siku hii masuala mbalimbali yajadiliwe na kufikia mazimio ikiwemo kujadili  haki zao za msingi katika kufanya kazi na kupata malipo, kupata elimu na mafunzo mbalimbali pamoja na kuwawezesha wajane na familia zao pamoja na kukemea vitendo vyote vya ukatili na unyanyasaji dhidi yao.

Pia Serikali zimeshauriwa kuchukua hatua na kuzingatia haki la kundi hilo hazivunjwi kwa kuzingatia sheria za wajane za kimataifa ikiwemo kukomesha aina zote za unyanyasaji kwa wanawake, watoto na kundi hilo la wajane.

Inaelezwa kuwa Kuna zaidi ya wajane 258 duniani huku wengi wao wakiishi katika dimbwi la umaskini, Mashariki mwa Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo imeripotiwa kuwa asilimia 50 ya wanawake ni wajane.

Tanzania inayokadiliwa kuwa na wajane zaidi ya Laki tano Serikali kwa kushirikiana na asasi mbalimbali za kiraia wamekuwa mstari wa mbele katika Kuhakikisha wajane wanapata haki zao za msingi bila dhuluma wala unyanyasaji.

Aprili 4, 2019 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alikutana na wajane wa Mkoa huo na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kunyimwa haki zao za kumiliki mali na unyanyasaji na takwimu za changamoto hizo zilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria marehemu Balozi. Agustine Mahiga ili zifanyiwe marekebisho na kuwaweka wajane katika mikono salama zaidi.

No comments: