FORUMCC WAIPONGEZA SERIKALI KWA JITIHADA ZAKE ZA UJENZI WA MITAMBO YA KUZALISHA UMEME UNAOTOKANA NA JOTO ARDHI

Mkurugenzi wa Shirika la FORUMCC Rebecca Muna(kulia) akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuhusu maoni yao katika bajeti ya fedha ya mwaka 20/21 ya Wizara ya Nishati ambayo imezingatia umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha matumizi ya nishati ya umeme itokanayo na jotoardhi. Kushoto ni Mratibu wa Miradi wa ForumCC Henry  Kazula.



Mratibu wa Miradi wa Shirika la ForumCC Henry  Kazula(kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa shirika hilo Rebecca Muna wakisikiliza maswali ya waandishi wa habari baada ya kutoa tamko lao la pongezi kwa Serikali kutokana na jitihada inazofanya katika ujenzi wa miundombinu ya umeme utokanao na jotoardhi.



Ofisa Miradi wa FORUMCC Sara Pima akitoa ufafanuzi kuhusu shirika hilo linavyochambua na kupitia bajeti mbalimbali za Serikali na hasa zinazohusu masuala ya nishati na mazingira.Kulia ni Rebecca Munna ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika hilo.

Baadhi ya wadau wa masuala ya mazingira wakiwa katia semina iliyoandaliwa na FORUMCC kwa ajili ya kuipitia bajeti ya Wizara ya Nishat .Semina hiyo imefanyika leo Juni 23,2020 jijini Dar es Salaam.

Wadau wa masuala ya mazingira na nishati jadidifu wakifuatilia mada wakati wa semina iliyoandaliwa na FORUMCC ambayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.



Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

SHIRIKA la FORUMCC ambalo linajihusisha na ushawishi wa kuchukua hatua stahimilivu na kupunguza athari za mabadiliko ya ya tabianchi limeipongeza Serikali kupitia ya Bajeti yake ya fedha ya Wizara ya Nishati ya 2020/2021kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme utokanao na jotoardhi katika mto Ngozi-Mbeya ifikapo 2021.

Limesema bajeti hiyo imechukua nafasi kubwa ya utekelezaji wa mwisho wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17-2020/21 ambayo imegusia vizuri na kufanyiwa maboresho katika upande wa Nishati jadidifu.

Mkurugenzi wa FORUMCC,Rebecca Muna leo Juni 23,2020 amewaaambia waandishi wa habari kuwa maoni yao kuhusu Bajeti iliyowasilishwa Bungeni hivi karibuni katika upande wa masuala ya Nishati ni inatia matumaini makubwa na wao kama wadau wanakilasababu ya kuipongeza Serikali.

Amefafanua katika bajeti ya mwaka huu imegusia vizuri masuala ya nishati jadidifu tofauti na miaka ya nyuma iliyopita."Awali hali ya uwekezaji wa upatikanaji wa umeme kwa ujumla, umeme utokanao na nishati ya upepo, jua na jotoardhi huchangia asilimia 3.8 tu ya kiwango cha nishati nchini.

"Tunaipongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme utokanao na jotoardhi katika mto Ngozi-Mbeya ifikapo 2021. Uzalishaji huo utachangia Megawati 30 katika jumla ya umeme unaozalishwa nchini pia, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme (MW 2.4) kutokana na nguvu ya upepo katika wilaya ya Mufindi-Iringa.

"Na kuanza kwa ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) katika mto Rufiji hii inaonyesha kwa namna gani Serikali hii imejipanga na kuweka nguvu katika kuimarisha nishaji jadidifu," amesema.

Ameongeza kuwa Septemba mwaka 2018, Serikali kupitia TANESCO ilitangaza fursa kwa wawekezaji binafsi katika miradi ya nishati jadidifu (Jua – MW 150 na Upepo – MW 200) lengo ni kupata miradi ya kuzalisha umeme wa jumla ya MW 950 kwa njia ya ushindani na kuingizwa katika Gridi ya Taifa,alisema.

Aidha alisema hadi kufikia mwezi Februari, 2019 tathmini ya zabuni kwa kampuni zilizoshiriki ilikamilika na taratibu nyingine zinaendelea na kwa mujibu wa bajeti 2020/21 miradi hiyo inaanza kutekelezwa mwaka 2020/21.

Muna amesisitiza kuwa uwekezaji zaidi wenye kipaumbele katika uzalishaji wa nishati jadidifu ulio rafiki kwa mazingira ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchangia ukuaji wa uchumi na jamii endelevu.

" FORUMCC chini ya Mradi wake wa masuala ya nishati jadidifu unaofadhiliwa na Shirika la Hivos imekuwa ikisaidia kusisitiza wadau mbalimbali umuhimu wa utumiaji wa nishati mbadala na kushauri serikali kuhakikisha masuala ya nishati jadidifu yanapewa kipaumbele ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,"amesema.

Wakati huo huo Mratibu wa Miradi wa ForumCC,Henry Kazula ametumia nafasi hiyo kueleza shirika lao na wadau mbali mbali wamekuwa mstari wa mbele kuishauri serikali kuhusu maboresho ya sera na uwajibikaji katika kuboresha hali ya upatikani wa nishati rafiki kwa mazingira na jumuishi ili kuchangia juhudi za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Ofisa Miradi Sara Pima amesisitiza wamekuwa wakielimisha jamii na kuwajengea uwezo asasi za Kiraia kuhusu fursa zilizopo za kiuwekezaji kupitia matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira katika kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

Amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia nishati jadidifu wakati huo huo tunawapa njia stahiki kuhimili na kukabiliana na athari za Mabadiliko ya tabianchi."Pamoja na mambo mengine tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii yetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira kama hatua mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi".

No comments: