DKT. BASHIRU AFAFANUA UKOMO WA WABUNGE, WAWAKILISHI NA MADIWANI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally leo tarehe 21 Juni, 2020 ameongoza mafunzo kwa Makatibu wa CCM wa mikoa na watumishi wa Makao Makuu, ambapo ametumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa ukomo wa wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa CCM.

Pamoja na mambo mengine, akifafanua suala hilo, Katibu Mkuu ameeleza kuwa ni vema Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa CCM wakaachwa waendelee kutekeleza majukumu yao kikatiba ikiwa ni pamoja na kuwa wajumbe wa vikao mbalimbali kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kutekeleza ahadi kwa wananchi kwa mujibu wa taratibu mpaka tarehe 14 Julai, 2020 dirisha la uchukuaji wa fomu za kugombea linapofunguliwa.

"Hoja ya Wabunge, Wawakilishi na madiwani kuendelea ama kutoendelea na kazi ni kuwa, wote hao bado wapo kazini, ukitaka Mbunge asiwe kazini maana yake Waziri Mkuu, Spika wote wasiwe kazini kwa sababu wote ni Wabunge, hatuwezi tukaacha ombwe la uongozi, nchi itaendeshwaje? Chama hiki sio cha uchaguzi ni Chama Cha Uongozi".

Amesisitiza kuwa, "Nasikia mnafukuzana huko kama digidigi na wabunge na madiwani eti kwa sababu ya kanuni, kanuni hazijawafuta kazi, wale ni wajumbe wa vikao vyote vya kazi na ni wawakilishi wetu wanatakiwa kufanya kazi ya Chama na kazi ya Umma mpaka tarehe 14 Julai, 2020 wanapochukua fomu".

Katibu Mkuu ameongeza kuwa, "Mbunge ama Muwakilishi anayehangaika siku mbili ama wiki mbili kabla ya uchaguzi mnahangaika naye wa nini, kama amedondoka atakusingizia wewe Katibu, alinizuia nisikutane na wananchi kumalizia ahadi zangu, kumbe alishajifia miaka minne iliyopita, unahangaika naye wa nini?".

Mafunzo hayo yanayoendelea Makao Makuu ya CCM Dodoma, yamehudhuriwa na Wajumbe wa Kamati Kuu  na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama Wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Saadaalla, Naibu Katibu Mkuu Bara Ndg. Rodrick Mpogolo, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndg. Pereira Silima na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga pamoja na Makatibu Wakuu wa Jumuiya zote tatu za CCM.

Semina ya leo ni muendelezo wa Mafunzo kwa Makatibu wa mikoa yote nchini pamoja ma watumishi wa makao makuu, iliyofunguliwa jana tarehe 20 Juni, 2020 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mzee Philip Mangula na itamalizika kesho Tarehe 22 Juni, 2020.

No comments: