WAKULIMA WILAYANI KAHAMA WAIOPONGEZA NFRA UNUNUZI WA MAZAO

WAKULIMA  wa wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga wameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuanza kuwajali wakulima wa Mazao mbalimbali kwa kuchukua hatua ya kuwakomboa kwa kutoa maelekezo ya kulielekeza shirika la Taifa la kuhifadhi chakula (NFRA) kununua mazao myote katika  msimu huu.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm Khamis Mgeja ambayo  inayojishughulisha na shughuli za Kilimo na ufugaji alipotembelewa na jopo la waandishi wa habari kwenye shamba lake la mpunga lililopo Kijiji cha Nyanhembe wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Mgeja amesema wakulima wamemsikia na kumuona hivi karibuni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akiwa mkoani Manyara akitoa maelekezo kwa kwa Shirika la Taifa la Kuhifadhi chakula ikiwemo na zao la mpunga na kuacha kasumba iliyozoeleka misimu iliyopita ya kununua zao moja la mahindi peke yake.

Aidha Mkurugenzi Mgeja amesema uamuzi huo wa Serikali utakuwa mwarobaini wa kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri katika mazao yao na kuwafanya wafanyabiashara wa mazao na baadhi ya walanguzi uchwara katika masoko nao watoe bei nzuri ya ushindani.

"Hivyo kumfanya mkulima anufaike na kilimo chake,kuna baadhi ya wakulima walianza kukata tamaa na kuchukua uamuzi mgumu wa kuachana na kilimo,"amesema Mgeja.

Akizungumzia shamba lake, Mgeja alieleza msimu huu amelima ekari 73 na kuongeza kuwa lengo lake kuu ni kulima ekari 250 katika kipindi cha msimu ujao huku akifafanua mafanikio na changamoto zinazowakabili wakulima  kwa ujumla na kushindwa kufikia malengo ni kutokana na  miundo mbinu mibovu.

Hata hivyo amemshukuru Mungu kwa kuwapatia mvua na kwwmba kwa msimu huu anatarajia kuvuna magunia 1,430 ya mpunga na hadi sasa anaendelea kuvuna na amefikisha gunia 320.

Mgeja ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Mkoa wa Shinyanga amesema  hivi sasa ameamua kupumzika siasa na mkkakati wake wa pili wa maisha yake amejielekeza kilimo na ufugaji.

Mgeja amesma kwa sasa amejipanga vizuri kwa kujielekeza katika sekta ya kilimo na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi na ufugaji wa nyuki na anatarajia kuchimba mabwawa ya kisasa kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji, ufugaji wa samaki, kilimo cha mpunga, mahindi pamoja na matunda.

Kuhusu changamoto zinazowakabili wakulima hao akiwamo na yeye amesema kuwa ni pamoja na ukosefu wa maghala ya kuhifadhia chakula, zana duni za kilimo, pembejeo ikiwemo ubora wa mbegu zinazopandwa.

Ametumia fursa hiyo kuziomba taasisi za fedha hasa benki ya kilimo kuwasaidia wakulima kuwakopesha kwa masharti ya riba nafuu, zana bora za kilimo ili kuweza kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo. “Wakulima wakiwezeshwa Tanzania bila njaa inawezekana kabisa na hata kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula la kwa Bara la Afrika.


“Nchi kama Thailand, Malasia, Singapore, Indonesia, Ucrain na India wamepiga hatua kubwa sana katika mapinduzi ya kilimo  kutokana na kuwa na zana za kisasa za kilimo pamoja na mfumo mzuri wa wa kilimo cha umwagiliaji,” amesema Mgeja.

Kwa upande wake mkulima Salima Kazinza ambaye ni mkazi wa Nyanhembe ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kutatua changamoto za miundombinu ya barabara inayoelekea katika mashamba yao."Ubovu wa barabara unaosababisha kubeba mazao kupitia baiskeli na begani ili kukwepa yasije kuozea shambani ukilinganisha mvua bado zinaendelea kunyesha".

Hivyo wakulima hao wanaiomba Serikali kuwatatulia changamoto hiyo ili kurahisisha usafiri wa kutoa mazao yao  wanayovuna na kuonyesha masoko.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba amesema kuhusu changamoto ya ubovu wa barabara kila mtu anafahamu msimu huu kulikiwa na neema ya mvua za masika, hivyo kutokana na mvua nyingi ilishindikana kufanya matengeneza ya miundombinu na kuahidi hadi mvua zitakapo katika.

“Kuhusu kilimo cha umwagiliaji nimeweka mazingira rafiki ambapo halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 14 kwaajili ya kufufua mabwa ya maji yatakayochimbwa katika Kata ya Isagehe, Mondo na Zongomera na baadae zoezi litaendelea kwa kata za Halmashauri ya Mji wa Kahama.s

'Niseme tu kuna changamoto ya maofisa kilimo kukosa usafiri lakini nimekaa kikao na mkuu wa idara ya kilimo na ufugaji na wamenihakikishia wamefanya ziara na kutoa ushauri na msimu huu nasubiri kuletewa takwimu ya ongezeko la mazao nilinganishe na misimu mingine iliyopita,” mesema Msumba.
 Khamis Mgeja akiendelea na shughuli za kilimo kwenye shamba lake wilayani Kahama mkoani Shinyanga
 Mgeja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nyanhembe Agricultural Farm akiendelea na shughuli za uvunaji wa mpunga katika shamba lake lililopo Kata ya Nyanhembe Kata ya Kilago Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga

No comments: