WAJUMBE KAMATI YA WAWAKILISHI CCM ZANZIBAR WATENGA MILIONI 33,000,000/- ZITAKAZOTUMIKA UTENGENEZAJI WA BARAKOA NA KUSAMBAZWA KWA WANANCHI
Mfanyabiashara Mohamed Ibrahim Raza akionyesha Uzalendo wake wa kukubali kusaidia mchango wowote utaohitajika na Serikali katika Ustawi wa Jamii Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akionyeshwa moja ya aina ya vitakasa mikono vilivyotolewa na Mfanyabiashara Mzalendo Nchini Mohamed Ibrahim Raza {Raza Lee} kusaidia mapambano dhidi ya kuangamiza Virusi vya Corona Nchini.Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mihayo Juma N’hunga.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga kati kati akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Misaada ya Diredt Aid na ule wa Manispaa ya Jiji la Zanzibar uliofika Ofisini kwake kutoa Mchango wa kusaidia mapambano dhidi ya Corona kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Naibu Waziri Mihayo Juma N’hunga akipokea msaada wa vyakula tofauti kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Misaada ya Direct Aid Dr. Ayman Mohamed Jamal kwa kushirikiana na Uongozi wa Baraza la Manispaa ya Jiji la Zanzibar.
Mheshimiwa Mihayo akimshukuru Mkurugenzi wa Taasisi ya Misaada ya Direct Aid Dr. Ayman Mohamed Jamal mada baada ya makabidhiwano ya mchango wa Vyakula kwa ajili ya Wananchi waliopata maambukizi ya Corona.Picha na – OMPR – ZNZ.
Wajumbe wa Kamati ya Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi ya Baraza la Wawakilishi wameamua kutenga Shilingi Milioni 33,000,000/- bakaa ya Fedha za Mfuko wa Kamati hiyo zitakazotumika katika utengenezaji wa Mask zitazosambazwa katika Majimbo yao ili kuwasaidia Wananchi kujikinga dhidi ya Virusi vya Corona.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa Taarifa hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kufuatia kumalizika kwa Kikao chao cha kawaida kilichopokea Taarifa ya Uwasilishwaji wa Mchango wao wa Shilingi Milioni 50,000,000/- zilizotolewa kuunga mkono nguvu za Serikali katika mapambano dhidi ya Corona.
Balozi Seif Ali Iddi alisema Wajumbe hao wameshateua Kamati itakayosimamia zoezi la utengenezaji wa Mask hizo kwa kutumia Viwanda vya ndani kwani mbali ya kupunguza gharama kubwa ya uagizaji wa vifaa hivyo kutoka nje ya nchi lakini pia mfumo huo wa kuwaamini wajasiri amali wa Ndani utasaidia kuongeza mapato kwa Viwanda hivyo.
Alisema Kamati hiyo ya Wawakilishi wa CCM ya Baraza la Wawakilishi bado ina jukumu la kuunga mkono kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na Serikali Kuu katika kuangamiza Virusi vya Covid – 19 ambavyo ni janga la Dunia kwa wakati huu.
Balozi Seif akiwa Msimamizi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwapongeza Wajumbe wa Kamati hiyo kwa uamuzi wao huo wa busara utakaoleta faraja kwa Jamii kutokana na wazo walilofikia la kutengeneza Vifaa vya Kinga.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alipokea msaada wa vifaa mbali mbali vilivyotolewa na Mfanyabiashara Mzalendo Nchini Mohamed Ibrahim Raza { Raza Lee}kwa ajili ya kusaidia nguvu za Serikali za kupambana na Corina.
Akipokea msaada huo uliojumuisha Sabuni, Ndoo za Maji pamoja na vitakasa Mikono{ Sanitizer} zilizotengenezwa hapa Nchini Balozi Seif aliendelea kuwashukuru Wafanyabiashara, Taasisi na Mashirika mbali mbali yaliyojitolea kuunga mkono jitihada za Serikali.
Alisema Serikali Kuu inaendelea kujenga matumaini kutokana na uelewa mkubwa wa baadhi ya Wananchi katika harakati zao za kila siku huku wakiwa makini na janga la Corona licha ya baadhi ya Watu kuendelea kukaidi baadhi ya maagizo yanayotolewa na Wataalamu wa Afya pamoja na Viongozi wa Serikali.
Akikabidhi msaada huo wa vifaa Mfanyabiashara Mohamed Ibrahim Raza {Raza Lee} alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yuko tayari wakati wowote kutoa mchango wake pale itakapohitajika kufanya hivyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokea mchango wa Tani 12 wenye Thamani ya Shilingi Milioni 21,000,000/- za Vyakula mbali mbali vilivyotolewa kwa pamoja kati ya Uongozi wa Taasisi ya Misaada ya Direct Aid kwa kushirikiana na Manispaa ya Jiji la Zanzibar.
Mchango huo wa Vyakula vitakavyosaidia Wagonjwa wa Corona walihifadhiwa wa matibabu huko Kidimni na JKU Mtoni ulipokelewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga kwa niaba ya Balozi Seif ndani ya Jengo la Ofisi hiyo Vuga Mjini Zanzibar.
Mh. Mihayo kwa niaba ya Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kupata faraja na kujenga matumaini kutokana na Taasisi na Mashirika tofauti ndani na nje ya Nchi kuendelea kuunga mkono jitihada za kupiga vita Virusi vya Corona Nchini.
Alisema si vyema kwa Taasisi, mashirika na Wadau wa misaada kama hivyo wakakata ghafla misaada yao wakati bado haijaeleweka hadi sasa matatizo ya janga la Corona yanamalizika lini ambayo mapambano yake yatawajibika kufanywa na kila Mtu hadi ukomo wake.
Wakitoa taarifa ya mchango huo Meya wa Jiji la Zanzibar Mstahiki Saleh Juma Kinana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Misaada ya Direct Aid Dr. Ayman Mohamed Jamal kwa pamoja walisema msaada huo ni muendelezo wa Ushirikiano uliopo kati ya Taasisi hizo na Serikali Kuu.
Walisema wao kama Viongozi wa Taasisi zao watajitahidi katika kuona yale malengo yao ya kusaidia ustawi na Maendeleo ya Umma unafika na kumgusa kila Mwananchi ndani ya Taifa hili.
Vyakula vilivyotolewa na kukabilidha kwa Kamati ya Kukabiliana na Maafa kwa pamoja kati ya Uongozi wa Baraza la Manispaa ya Jiji la Zanzibar na Taasisi ya Misaada ya Direct Aid ni pamoja na Mchele, maharagwe, Mafuta ya Kupikia, Unga wa Ngano pamoja na Sukari.
No comments: