UWT DODOMA MJINI YATOA VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONA KATIKA KITUO CHA WAGONJWA WA UKOMA
Mmoja wa Walemavu wa Ugonjwa wa Ukoma ambao wanaishi katika kituo cha Samaria jijini Dodoma akinawa kwa maji yanayotiririka baada ya Umoja wa Wanawake Tanzania wilaya ya Dodoma Mjini kupitia Katibu wake, Diana Madukwa (mwenye shati la kijani) kukabidhi vifaa vya kujikinga na Corona kwenye kituo hiko.
Katibu wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa akionesha baadhi ya vifaa vya kujikinga na Corona na vyakula ambavyo UWT imepeleka kama msaada kwenye kituo cha Samaria wanapoishi watu wenye ulemavu wa ugonjwa wa Ukoma jijini Dodoma leo.
Katibu wa UWT Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa akizungumza na wananchi wanaoishi kwenye kituo cha Samaria baada ya kufika na kukabidhi msaada wa vifaa vya kujikinga na Corona pamoja na mahitaji ya kibinadamu ikiwemo vyakula.
Hili ni bonde ambalo wananchi hao wenye ugonjwa wa Ukoma inawalazimu kuvuka ili kwenda kwenye makazi yao pindi. Wameiomba serikali iwasaidie kupata barabara nzuri.
Charles James, Michuzi TV
KATIBU wa Umoja wa Wanawake Tanzania Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa ametoa onyo kwa watu wanaokula misaada inayotolewa na wadau mbalimbali kwa watu wenye ulemavu.
Ametoa onyo hilo leo wakati alipotembelea kituo cha walemavu wa ugonjwa wa Ukoma kilichopo Tarafa ya Hombolo jijini Dodoma na kutoa misaada mbalimbali ya vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona pamoja na mahitaji ya kibinadamu.
Akizungumza na viongozi na wananchi wanaoishi katika kituo hiko, Madukwa amesema ni jambo la ajabu kuona wapo viongozi waliochaguliwa na wananchi lakini wanahusika kula misaada inayotolewa kwa watu wenye uhitaji.
Madukwa amemuuagiza uongozi wa mtaa huo na kituo wanachoishi walemavu hao kuhakikisha msaada huo wa vifaa vya kujikinga na Corona pamoja na vyakula walivyoleta vinagaiwa kwa wahusika wenyewe ambao ni watu wenye Ukoma.
" Ni jambo la ajabu sana kusikia ndugu zetu wenye ulemavu wanalalamika kwamba wanapoletewa mahitaji na wadau basi misaada hiyo hugaiwa pia kwa watu ambao siyo walemavu.
Nauagiza uongozi wa Mtaa pamoja na uongozi wa Kituo hiki kuhakikisha vitu hivi vinavyoletwa hapa ikiwemo hivi ambavyo sisi UWT tumeleta vinawafikia walengwa wenyewe bila kuchakachuliwa," Amesema Madukwa.
Katibu huyo amesema vifaa vya kujikinga na Corona ambavyo wamevipeleka kituoni hapo ni pamoja na Barakoa 300, Ndoo za Kunawia Mikono 15 na sabuni zake lakini pia wamepeleka Mchele, Sukari na Mafuta ya kupikia ambavyo vyote hivyo vitagaiwa kwa kaya 35 ambazo ni za walemavu wa Ukoma.
Amesema atahakikisha yeye mwenyewe anafuatilia kujua kama wananchi hao wamepata misaada hiyo kwa haki na kama kutakua na aina yoyote ya uchakachuaji basi wahusika watapelekwa kwenye vyombo vya sheria.
" Ndugu zangu sisi UWT Wilaya ya Dodoma Mjini tumefika hapa kuwaletea vifaa hivi vya kujikinga na Corona kwa sababu tunathamini nafasi yenu na tunajua kwamba mnahitaji kupewa vifaa hivi kwa ajili ya kujikinga na maambukizi.
Chama cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Rais Dk John Magufuli tunaamini katika haki na usawa kwa kila mwananchi hivyo hatuwezi kukubali kuona wenzetu nyinyi mnabaguliwa au mnanyang'anywa haki yenu, hii misaada yote inayokuja hapa ni lazima iwafikie walengwa ambao ni nyinyi," Amesema Madukwa.
Amewataka viongozi wa kituo hiko pia kusaidia kutoa elimu kwa wananchi hao juu ya kujikinga na ugonjwa huo lakini pia akiwasihi kuondoa hofu kama ambavyo Rais Magufuli amekua akisisitiza huku wakichukua tahadhari kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Madukwa pia ameahidi kuendelea kushirikiana na kituo hicho katika kuwahudumia wananchi hao na kwamba amepokea changamoto za ubovu wa miundombinu ya barabara na ukosefu wa umeme na kuahidi kuzipeleka kwenye mamlaka za kiserikali ili zitatuliwe.
Kwa upande wake Mlezi wa Kituo hiko kutoka Taasisi ya LFSC, Dk Philemon Ulanga ameishukuru UWT Wilaya ya Dodoma Mjini kwa kukikumbuka kituo hiko na kuwaletea vifaa vya kujikinga na Corona pamoja na mahitaji ya kibinadamu kama Chakula.
" Kituo hiki kina kaya 35 na jumla ya wananchi 300, kuna changamoto nyingi sana hapa lakini kubwa ni barabara na umeme, watu hawa wengine hawawezi kutembea na wengine hawana vidole vya kuwashia vibatari lakini umeme ukija na barabara tunaamini changamoto zingine zitakua zimepungua," Amesema Dk Ulanga.
Nae Simon Joseph mmoja wa walemavu ameishukuru UWT kwa kufika na kuwapa misaada hiyo kwani itakua chachu ya wao kujikinga na maambukizi ya Corona kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza.
No comments: