UVUMILIVU WA SIMBACHAWENE, DK MWIGULU NA REKODI ZAO ZA KIBABE KWENYE SERIKALI YA MAGUFULI
Charles James, Michuzi TV
UNAMUELEWA Rais Dk John Magufuli?. Mimi namuelewa sana. Rais mchapakazi, asiye na utani, mwenye hofu na Mungu. Zaidi anafuata kanuni ya samehe mara saba sabini. Utanielewa tu.
Sogea hapa: Katika kitabu cha 48 Laws of Power kilichoandikiwa na Gwiji, Robert Greene, Sheria namba moja inasema, " Never Outshine your Master"
Tafsiri isiyo rasmi ni kwamba, "Usijifanye unajua kuliko Kiongozi/Bosi wako. Hata kama kweli unajua zaidi yake, usioneshe hilo hadharani. Onesha utii na unyenyekevu kwake.
Tuendelee kuelewana tu taratibu. Septemba 2017, Rais Dk John Magufuli alitengua uteuzi wa George Simbachawene ambaye alikua ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi.
Hii ilikuwa ni baada ya jina la Simbachawene kutajwa kwenye ripoti za Bunge za Madini ya Almasi na Tanzanite. Rais Magufuli akaagiza wateule wake waliotajwa kwenye ripoti hiyo wakae pembeni.
Simbachawene na aliyekua Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani wakawekwa pembeni baada ya wenyewe kuandika barua ya kujiuzulu kama Rais alivyoagiza.
Kutokea 2017 Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe, Dodoma na Waziri katika nafasi mbalimbali kwenye Serikali ya awamu ya nne alikua kimya akijitafakari.
Pale ilipombidi kusimama bungeni kuisemea Serikali ya Chama chake alisimama na kusema. Alipotakiwa kuitetea serikali yake alifanya hivyo.
Hakugeuka kuwa mkosoaji wa Rais na Serikali kama wengine wanaotumbuliwa hufanya.
Hakujifanya anajua kama wengine. Hakuitisha 'press' na wandishi wa habari baada ya kutumbuliwa. Alifahamu Rais ni mmoja, Boss ni mmoja na ndio mwenye mamlaka ya kuteua na kutengua. Alimpa heshima Rais.
Simbachawene angeweza kuita vyombo vya habari na kujisafisha baada ya jina lake kukutwa kwenye ripoti ile. Angeweza kujitetea kwa namna yoyote ile ili kuonekana msafi. Hakuthubutu. Akakaa kimya.
Alifahamu fika kitendo cha jina lake kutajwa kilikua kumuondolea sifa zake mbele ya Rais na wananchi wake. Hivyo njia pekee ni kukaa kimya na kujitafakari. Kuomba msamaha na kutengeneza uaminifu wake tena kwa Taifa.
Kwa Mbunge yeyote wa Chama cha Mapinduzi hupaswi kuwa na haraka wala kuumia unapotumbuliwa. Iwaingie akilini kila Mbunge wa CCM ni Waziri mtarajiwa.
Simbachawene alilijua hili akaamua kutulia zake kimya.
Na kwa sababu anafahamu Rais Magufuli ni mwenye kusamehe. Hakuona kama anapungukiwa chochote kutulia kimya na kuwa mvumilivu baada ya kuondolewa kwenye Uwaziri wake.
Alisimama mara zote bungeni kuitetea serikali, alisimama mara zote kuwakumbusha watanzania miradi mikubwa ya Afya, Miundombinu, Elimu ambayo Rais Magufuli anaitekeleza.
Alizieleza sifa za Kiongozi wake badala ya kujifanya anajua kwa kukosoa kama wengine.
Julai 2019. Baada ya kupita miaka miwili, Rais Magufuli anamrudisha Simbachawene kwenye Baraza lake la Mawaziri kwa mara ya pili.
Hii ni baada ya uteuzi wa January Makamba kama Waziri wa Mazingira kutenguliwa. Simbachawene anaweka rekodi ya kuwa Waziri wa kwanza kutumbuliwa na kisha kurudishwa tena kwenye utawala wa Rais Magufuli.
Januari 2020, Rais Magufuli anamteua tena Simbachawene kutoka kuwa Waziri wa Mazingira na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya uteuzi wa Kangi Lugola kutenguliwa.
Kwa mara nyingine tena, Simbachawene anaweka rekodi ya kuwa Waziri wa kwanza kuhudumu Wizara tatu tofauti ndani ya kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya Rais Magufuli.
Hayo yote yametokea kwa sababu ya utii, nidhamu na uvumilivu. Simbachawene ametoa majibu ya mambo hayo matatu.
NI DK NCHEMBA TENA
Mei 2, Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inatangaza uteuzi wa Dk Mwigulu Nchemba uliofanywa na Rais wa kuwa Waziri wa Sheria na Katiba.
Dk Nchemba anateuliwa kushika nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Dk Augustine Mahiga ambaye alifariki mwishoni mwa wiki jana.
Hii inakua mara ya pili kwa Mwigulu kurejea kwenye Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.
Nikukumbushe tu, Mwigulu alitumbuliwa kwenye nafasi yake ya Uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Rais Magufuli Julai 2018 na nafasi yake kuzibwa na Kangi Lugola.
Baada ya Mwigulu kutumbuliwa alirudi Jimboni kwake na kuzungumza na wananchi wake waliomchagua kuwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi.
Akatoa shukrani zake kwa Rais Magufuli kwa kumuamini kwenye serikali yake. Mwigulu hakuonesha kinyongo cha kuondolewa Uwaziri wake kwa Rais. Hakukimbilia Twitter wala Instagram kurusha madongo. 'Alikausha'.
Mara zote amekua ni mtu wa kuisemea serikali kwa kuwakumbusha wananchi mambo makubwa ya kimaendeleo ambayo yamefanywa ndani ya kipindi cha muda mfupi.
Angeongelea Ujenzi na faida za mradi wa Reli ya kisasa, kesho angezungumzia ujenzi wa vituo zaidi ya 300 vya Afya vilivyojengwa na Rais Magufuli ndani ya kipindi kifupi.
Mwigulu hakusita kuwakumbusha watanzania kwamba Rais pia anatoa elimu bila malipo kuanzia Shule ya Msingi hadi kidato cha nne.
Ni Dk Nchemba huyu ambaye mara kadhaa amekua akiraruana kwa hoja na wapinzani mitandaoni pale walipojaribu kusema mambo ya 'uongo' dhidi ya serikali ya Chama chake. Hakua nyuma kujibu hoja za wapinzani.
Leo hii ameteuliwa tena kuwa Waziri. Maana yake imani aliyoivunja kwa Rais Magufuli amefanikiwa kuirudisha tena. Hii ni kwa sababu Rais hakukosa jina la Mtu mwingine badala yake alimfikiria Nchemba.
Huu ni uthibitisho kwamba JPM husamehe.
Chukua hii pia. Mwigulu nae amefikia rekodi ya Simbachawene ya kuhudumu Wizara tatu tofauti kwenye serikali ya Rais Magufuli.
Mwanzoni Rais alimteua Mwigulu kuwa Waziri wa Kilimo kabla ya kumuhamishia Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya Charles Kitwanga kutumbuliwa. Juzi amempa Wizara ya Sheria na Katiba. Hii ni rekodi ya kibabe sana.
Niseme tu Mawaziri hawa wote wawili kwa pamoja wametoa elimu kubwa sana kwa wanasiasa wengi wa Nchi hii, hasa vijana.
Tujifunze kuwa na utii, nidhamu na uvumilivu. Nafasi bado iko kwako ambaye leo umeondolewa kazini. Kila Mbunge wa CCM ni Waziri mtarajiwa. SOMO!
0683 015145
No comments: