USIMAMIZI NA UTEKELEZAJI WA SHERIA KUYAWEKA SALAMA MAZINGIRACYETU

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO-DAR ES SALAAM


MAZINGIRA yanatajwa kuwa ni mojawapo ya chanzo kuu cha maendeleo ya sekta zote za uzalishaji mali na ukuaji uchumi wa taifa lolote duniani na hivyo kuwa rasilimali muhimu kwa ajili ya mahitaji ya sasa na vizazi vijavyo.
Katika miaka ya hivi karibuni imedhihirika kuwa mazingira yetu si salama kutokana na shughuli zisizo endelevu zinavyochangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira na kusababisha uharibifu wa ardhi, uchafuzi wa mazingira n.k.
Maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kutunza mazingira, na ushahidi huo ni pamoja na kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame, mafuriko na kuongezeka kwa matumizi ya zebaki katika sekta ya madini hususani wachimabji wadogo wa dhahabu.
Mara nyingi tumeshuhudia katika uzalishaji wa viwanda, mazingira asilia huharibiwa sana, hususan kwa taka zitokanazo na uzalishaji na utupwaji wake unaopelekea kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira asilia, hususan ardhi na hewa.
Pamoja na Serikali kuchukua jitihada kubwa katika utunzaji na usimamizi wa mazingira, hali ya mazingira nchini bado si ya kuridhisha, hali inayochangiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa rasilimali watu wa kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura 191 katika ngazi zote.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu anasema katika mwaka 2019/20, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamzi wa Mazingira ( NEMC) limefanya ukaguzi katika miradi ya kijamii na kiuchumi.
Anaongeza kuwa katika ukaguzi huo jumla ya miradi 1,132 ilifanyiwa tathmini ya uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira nchini ili kuangalia iwapo inaweza kuwa na athari kwa mazingira.
‘Katika kipindi hiki, Baraza limepokea malalamiko 257 kuhusu uchafuzi wa Mazingira na kufanya ufuatiliaji kuhusu malalamiko hayo, ambapo ukaguzi uliofanyika ulibaini changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwemo kutiririsha majitaka kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu’’ anasema Zungu.
Waziri Zungu anazitaja changamoto nyingine ni pamoja na Matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali kama misitu ya asili kwa ajili ya kuni na ujenzi, Ukosefu wa mifumo ya kuhifadhi taka ngumu, Uzalishaji wa hewa chafu, Uzalishaji na usambazaji wa mifuko mbadala isiyokidhi viwango.
Akifafanua zaidi Zungu anasema NEMC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Jeshi la Polisi limetoa maagizo na maelekezo ili kukabiliana na changamoto hizo na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufungua mashitaka ya uchafuzi wa mazingira, amri za katazo na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ya Mazingira na Kanuni zake.
Anaongeza kuwa Amri na makatazo 79 kwa wavunja sheria ya mazingira zimetolewa na kufuatiliwa pamoja na kuendelea kusimamia kesi 12 zinazohusu makosa mbalimbali ya kimazingira.
Aidha Zungu anasema katika mwaka 2019/2020, Serikali pia ilifanya mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM), usajili wa miradi na utoaji wa vyeti vya mazingira kwa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi nchini ili kujiridhisha na viashiria vya madhara na ubainishaji wa awali wa athari za mradi.
Anasema katika mwaka wa fedha 2019/20, Baraza limesajili jumla ya Miradi 887 ikiwemo miradi 556 ya Tathmini za Athari kwa Mazingira (TAM) na miradi 331 ya kufanyiwa Ukaguzi wa Athari za Mazingira, ikiwa ni asilimia 74 ya miradi ambayo imekusudiwa kufanyiwa mapitio kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20.
Waziri Zungu anasema katika mwaka 2019/2020 pia jumla ya miradi ipatayo 375 imepata vyeti vya mazingira, ambapo miradi 225 ni miradi ya Tathmini za Athari kwa Mazingira na Miradi 150 ya ukaguzi wa Athari za Mazingira na miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za upembuzi.
Afya, ustaarabu na ustawi wa taifa letu kwa ujumla vinategemea sana hali mazingira yanayotuzunguka, uchafuzi wa mazingira unaathari kubwa kiafya hasa katika uenezwaji wa magonjwa ya mlipuko, na kuilazimu serikali kutumia gharama kubwa katika uwekaji wa miji katika mazingira ya usafi.
Mazingira safi ni maisha yetu, mazingira safi ni uhai wetu, mazingira safi ni afya yetu, mazingira safi ni uchumi wetu hivyo kila mmoja wetu ajitafakari namna anavyoweza kuwa na mchango chanya katika kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi.

No comments: