TRUMP AINYUKA WHO WARAKA MZITO


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

RAIS wa Marekani Donald Trump ameendelea kulituhumu Shirika la afya Duniani (WHO) kwa kushindwa kuwa chombo huru katika kupambana na janga la mlipuko wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19.) Ambavyo hadi sasa vimesambaa duniani kote na hakuna chanjo wala kinga iliyopatikana hadi sasa.

Kupitia barua aliyoiweka katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiielekeza kwa Mkurugenzi wa WHO Dkt. Tedros Adhonom Ghebreyesus Trump amesema, aliamua kusitisha michango ya nchi yake kwa Shirika la Afya Duniani( WHO) tangu Aprili 14 mwaka huu ili kufanya uchunguzi juu ya mambo ambayo anadai WHO ilizembea kuyafanya katika kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona (Covid 19.)

Pamoja na mambo mengine mengi Trump anasema uchunguzi umebaini yafuatayo;

 WHO haijatoa taarifa kwa wakati hasa kwa kutangaza kuwa virusi vya Covid-19 kuwa janga la ulimwengu.

Pia ameeleza kuwa WHO imetoa taarifa za uongo na za kuaminisha dunia kwamba Covid -19 haiambukizwi kwa mtu na mtu licha ya baadhi ya wataalamu kueleza namna ya virusi hivyo vinavyosambaa.

Vilevile amesema kuwa WHO haikufanya utafiti wake kwa uhuru kupitia wataalamu wake na badala yake wakategemea taarifa za China na kuihabarisha dunia jambo ambalo huenda ilikuwa upotoshaji.

Aidha amelituhumu shirika hilo kwa kuendelea kuisifu China kwamba wanafanya kazi nzuri hata baada ya wao kuzuiwa kufika Wuhan kwenye kitovu cha ugonjwa mapema badala yake kuruhusiwa mwishoni kabisa ambapo ugonjwa ukiwa umeshaenea dunia nzima.

Waraka huo umeeleza kuwa WHO haikuwaonya China juu ya ubaguzi na unyanyasaji wa watu weusi  wanaoishi China  kwa madai kwamba ndio waliosababisha kuenea kwa Virusi vya  Corona na hiyo ni baada ya mabalozi wa nchi za Afrika kuandika barua kwa Serikali ya China kuhusiana na ubaguzi wa wananchi wa mataifa ya Afrika.

Kupitia waraka huo pia imeelezwa kuwa WHO iliikosoa USA kwa kuzuia wachina kuingia Marekani wakati huohuo ikiisifu China kwamba inalinda Dunia.

Zaidi sana Trump amemlaumu mkurugenzi wa WHO kwa kutoonyesha uwezo kama mtangulizi wake ambaye mwaka 2003 aliongoza Dunia kupambana na mlipuko wa homa ya Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS) ambapo aliionya China kuacha kutoa taarifa za kupotosha ambazo zitahatarisha usalama wa ulimwengu.

Hivyo Trump ametoa siku 30 kwa WHO kujirekebisha vinginevyo ataondoa kabisa bajeti yake ya kuchangia WHO na atafikiria kama kuna umuhimu wa kuendelea kuwa mwanachama tena kwa sababu hawezi kutumia pesa za walipa kodi wake kwenye mradi ambao hauna maslahi.
RAIS wa Marekani Donald Trump

No comments: