SHIRIKA LA SEMA LATOA ELIMU YA KUJIKINGA NA CORONA KWA ASKARI POLISI WA MKOA WA SINGIDA

Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa akitoa elimu ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kwa Askari Polisi wa Kituo Kikuu cha Mkoa wa Singida leo hii Asubuhi.
Askari Polisi wa Kituo Kikuu cha Mkoa wa Singida, wakipata elimu hiyo.
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Florence Mwenda, akisisitiza jambo kwa askari wa kituo hicho, wakati wa kutolewa kwa elimu hiyo.
Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa, akisisitiza jambo wakati akitoa elimu hiyo.
Maafisa wa Shirika lisilo la Kiserikali la Sustanable Environment Management Action (SEMA) la Mkoa wa Singida, Gerson Janga (kushoto) na Witness Anderson wakitoa elimu hiyo kwa askari hao kwa njia ya mabango.
Askari hao wakiwa wamesimama kwa tahadhari ya kuacha mita zaidi ya moja kama njia ya kujikinga na maambukizi ya Corona.

Na Dotto Mwaibale,Singida
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Sustanable Environment Management Action (SEMA) kwa kushirikiana na wadau kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya wamtoa elimu ya kujikinga dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kwa Askari Polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Singida leo hii Asubuhi.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Mdau wa mapambano dhidi ya Corona kutoka Taasisi ya Empower Youth Prosperity ( EYP) ya mkoani Mbeya, Ipyana Mwakyusa alisema elimu hiyo ililenga kukumbusha namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

"Kila mtu anajua uwepo wa ugonjwa huu tunatoa elimu hii kwenu kwa ajili ya kukumbusha tukizingatia nyie wenzetu huwa mnakutana na watu wengi" alisema Mwakyusa.

Akielezea jinsi ya kujikinga na homa ya Virusi vya corona Mwakyusa alitoa tahadhari kwa askari hao kukaa mbali angalau mita 1 au 2 na mtu wakati wakiwa kazini.

Tahadhari nyingine alioitoa ni pamoja na kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kutumia kitambaa safi au sehemu ya mbele ya kiwiko cha mkono, kuepuka kugusana, kusalimiana kwa kushikana mikono.

Tahadhari nyingine ya jinsi ya kujikinga pamoja na mambo mengine ni kuepuka kugusa macho, pua au mdomo baada ya kunawa. 

"Safisha mikono yako mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kwa dawa ya kutakasa mikono" alisema Mwakyusa.

Akizungumzia ugonjwa huo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Florence Mwenda, alisema kwa upande wao wamechukua tahadhari zote za kujikinga pamoja na watu wanao wahudumia.

Kampeni ya utoaji wa elimu hiyo inafanywa kwa ufadhili wa Shirika la Stromme East Africa Foundation lenye Makao Makuu Kampala nchini Uganda huku ufadhili mkuu wa mashirika hayo ukitolewa na Shirika la Stromme Foundation la Norway kupitia mradi wa uwezeshaji jamii kiuchumi unaowalenga vijana wa kiume, wa kike, watoto na wakina mama.

No comments: