PLAN INTERNATIONAL WAKABIDHI VIFAA VYA KUKABILIANA NA CORONA WILAYANI KISARAWE...DC JOKATE ATOA NENO

 Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo(kulia) na Meneja wa Shirika la Plan International (kushoto) katika Wilaya hiyo Marcely Madubi(kushoto) wakioneshwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani  Stanphod Mwakatabe moja ya vifaa vya msaada ambavyo vimetolewa na Shirika hilo kwa ajili ya mapambano dhidi ya Corona ndani ya wilaya hiyo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Jokate  Mwegelo akiwa ameshika taulo za kike ambazo zimetolewa na Shirika la Plan International kwa ajili ya wanafunzi wa kike ndani ya Wilaya hiyo ambao kwa sasa wako nyumbani baada ya shule kufungwa kutokana na janga la Corona.Aliyeshika kipaza sauti ni Meneja wa Shirika la Plan International Wilaya ya Kisarawe Marcely Madubi

 
Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani akifafanua jambo baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali vya kukabiliana na Corona vyenye thamani ya Sh.milioni 76.8.
 
Katibu Tawala Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Tella Mwampamba (aliyesimama) akizungumza kabla ya Shirika la Plan International kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vyenye zaidi ya Sh.milioni 76.8 kwa ajili ya kukabiliana na Corona katika Wilaya hiyo.
 
: Meneja wa Shirika la Plan International Wilaya ya Kisarawe Marcely Madubi akifafanua kuhusu msaada wa vifaa mbalimbali vya kukabiliana na Corona ambavyo wamevitoa kwa ajili ya Wilaya ya Kisarawe.
 
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani  Stanphod Mwakatabe(aliyesimama) akielezea umuhimu wa vifaa vya kukabiliana na Corona ambavyo vimetolewa kwa ajili ya kuwezesha watoa huduma za afya katika Wilaya hiyo kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia wagonjwa bila ya kupata maambukizi.
 
Sehemu ya matanki ya maji ya ujazo wa lita 500 kila moja ambayo yametolewa na Shirika la Plan International kwa ajili ya kuiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kukabiliana vema na janga la Corona ambapo matanki hayo yatagawiwa kwenye vituo vyote vya afya wilayani Kisarawe.
 
Meneja wa Shirika la Plan International Wilaya ya Kisarawe Marcely Madubi akifungua moja ya boksi lenye vifaa vya vipima joto kwa ajili ya kumuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo.
Meneja wa Shirika la Plan International Wilaya ya Kisarawe Marcely Madubi akifungua moja ya boksi lenye vifaa vya vipima joto kwa ajili ya kumuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo.




Said Mwishehe, Michuzi TV

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani limekabidhiwa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh.milioni 76.8 kwa ajili ya kukabiliana na janga la Corona kutoka Shirika la Plan International.

Msaada huo umekabidhiwa na Meneja wa Shirika hilo Kisarawe Marcely Madubi kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo ambaye ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa vita dhidi ya Corona Tanzania imefanikiwa kushinda kwa asilimia kubwa.

Vifaa hivyo ambavyo idadi yake ipo kwenye mabano ni vipima joto vya mionzi(8), matenki ya maji yenye ujazo wa Lita 500(20), glovu boksi (80),galoni za lita tano za vitakasa mikono (5), vitakasa mikono (210), aproni (80), barakoa FFP2 (30), maboksi ya taulo za kike (100), miwani za kujikinga (30), viatu (120), vifuniko vya mwili (10), mabango (18) na vipeperushi (1500) kwa ajili ya kusambaza elimu.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo leo katika Hospitali ya Walaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mkuu wa Wilaya hiyo Jokate Mwegelo amelishukuru shirika hilo kwa msaada walioutoa ambao utasaidia kuimarisha mapambano ya Corona.

"Plan International kwa kushirikiana na Shirika la Champion Chanzige (CCO),wametoa msaada wa vifaa hivi pamoja na kutoa elimu kwa njia ya matangazo kwa jamii itakayoambatana na wasanii wa wilaya yetu kundi la Kibajaji, kwa kuzunguka kata 17.Utoaji huo wa elimu utakwenda sambamba na ugawaji aa vipeperushi na ubandikaji wa mabango katika ofisi za kata na maeneo mengine muhimu,"amesema.

Pia alisema Shirika la Plan International litawezesha mafunzo kwa wataalam na viongozi wa ngazi ya wilaya, kata na vijiji wapatao 488 pamoja na kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuandaa vipindi vitakavyotoa elimu rafiki kwa watoto kupitia runinga na redio.

Jokate ametumia nafasi hiyo kuiomba jamii ya Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha inamlinda mwanafunzi wa kike hasa kipindi hiki ambacho wako majumbani ili kuwaepusha kupata mimba kwani Serikali inatumia gharama kubwa ya uwekezaji kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu, hivyo waachwe watimize ndoto zao.

Pia ameeleza namna ambavyo Wilaya hiyo imefanikiwa katika mapambano dhidi ya Corona na kubwa zaidi Tanzania imefanikiwa kushinda vita dhidi ya ugonjwa huo kutokana na maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Rais Dk.John Magufuli kuhusu mbinu bora na sahihi za kuukabili ugonjwa huo.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Plan International Madubi amefafanua jumla ya msaada wote ambao wameutoa kwa ajili ya Wilaya ya Kisarawe una thamani ya Sh.milioni 76.8 na katika fedha hizo kuna mgawanyo kulingana na aina ya msaada ambao wameutoa.

Amesema kuwa vifaa vilivyotokewa kwa ajili ya hospitali vina jumla ya thamani ya Sh. milioni 34.2 na Sh. milioni 42.5 zitatumika kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii dhidi ya Corona, kukarabati gari la wagonjwa na kuendesha mafunzo wataalam wa afya, walemavu, viongozi wa dini na wa serikali wapatao 488.

"Tunaamini vitakasa mikono, sabuni na matenki ya maji yatakayowekwa vituo vya afya na shule tunazotekeleza ujenzi wa vyoo na madarasa vitasaidia jamii na maeneo hayo kujikinga na maambukizi ya Corona. Maboksi 100 ya taulo za kike zitasaidia wasichana wapatao 1,200 hususan waishio kwenye mazingira magumu," amesisitiza.

Pia Madubi amewaomba wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawaondoa watoto kwenye hali ngumu ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia na kubebeshwa majukumu mengine ya kifamilia badala ya kujisomea. Ametoa rai kwa jamii kuwa licha ya wanafunzi kuwa wako nyumbani lakini wanatakiwa kuendelea kusoma kwa kujisomea kila siku ili kutosahau waliyofundishwa shuleni kabla ya Corona kuingia nchini

No comments: