Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir atembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, awapongeza wataalamu
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam .
MUFTI Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir ameitembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kuwapongeza wataalamu wake kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania, licha ya kuwapo janga la ugonjwa wa Corona.
Sambamba na hilo, Mufti Zubeir amewajulia hali wagonjwa na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili hali zao zizidi kuimarika baada ya kufanyiwa matibabu dhidi ya matatizo ya moyo yaliyokuwa yakiwakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mufti Zubeir aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kwa kuhakikisha watanzania wanaendelea kuchapa kazi huku wakizingatia maelekezo muhimu yaliyotolewa na watalaamu wa afya kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, jinsi ya kujikinga wasipate maambukizi ya virusi hivyo.
“Watanzania ni muhimu sana waendelee kufuata maelekezo ya wataalamu ya kujikinga dhidi ya tatizo hili la Corona, tumeelezwa ugonjwa upo nchini mwetu, tukiendelea kushikamana, na kuamini yakuwa Mwenyezi Mungu atatusaidia tutavuka salama”.
Aliongeza , “Madaktari na wauguzi kuwahudumia wagonjwa ni sadaka ambayo Mungu mwenyewe amewachagua watu wa namna hii, nawasihi waendelee kusaidia watu pale wanapohitaji tiba, wasiwakimbie,”alisema.
Aidha Mufti Zubeir waliwataka watanzania waondoe hofu, maana hofu ni moja ya magonjwa makuu duniani, “Ukiwa na hofu nguvu za Mwenyezi Mungu zinapotea, sisi katika uislamu tunafundisha watu wasiwe na hofu, Watanzania wasiwe na hofu, wasimame imara”, alisisitiza.
Mufti Zubeir aliongeza yakuwa yalishapita magonjwa mengi makubwa kama haya, yakachukua maisha ya watu wengi lakini watu walisimama imara, magonjwa yakaondoka, imebaki historia.
“Ninampongeza mno Prof. Janabi, wataalamu wa JKCI na wataalamu wote wa afya Tanzania kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha watanzania wanaendelea kuwa na afya njema na kuendelea na maisha yao kama kawaida,” alisisitiza.
Kuhusu juhudi mbalimbali zinazofanyika kwa njia ya tafiti ya kutafuta chanjo au dawa dhidi ya Corona, Mufti Zubeir alisema ni jambo linaloleta faraja na matumaini makubwa.
“Naona kuna msaada mkubwa sana, hatuna uwezo mkubwa kwa nchi yetu ndogo kama hii, hatukuweza kufikiri kufika hapa, tunaona Mungu ametusaidia, wataalamu wetu wameweza kufikia katika vumbuzi mbalimbali kupata dawa, hii inaleta matumaini.
“Hata ile tafsiri ya dua niliyoifanya kwa wagonjwa niliokuja kuwaona hapa si tu kuondoa ugonjwa moja kwa moja bali pia kuwafanya wataalamu wetu kupata fikra, vumbuzi na gunduzi za kufanya tafiti za kina kuweza kupata dawa na kuutibu ugonjwa huu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar bin Zubeir kwa kuweza kufika JKCI kuwaombea dua wagonjwa wa moyo waliolazwa katika Taasisi hiyo.
“Ujio wa Mufti Mkuu Tanzania Sheikh Zubeir umewapa faraja kubwa wagonjwa waliolazwa katika taasisi yetu, hii inaonyesha kuwa viongozi wa dini wanawakumbuka wagonjwa waliolazwa na kuwaombea dua ili waweze kurejea katika afya njema kama walivyokuwa kabla hawajaanza kuugua,” alisema Prof. Janabi.
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar bin Zubeir akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi mara baada ya kumaliza kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kuwaona wagonjwa waliolazwa pamoja na kuwaombea dua ili wapate uponaji wa haraka.Picha na JKCI.
No comments: