MKURUGENZI HALMASHAURI YA MWANGA AFUNGUKA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO, AWAITA WAWEKEZAJI KUWEKEZA KWENYE UTALII


Charles James, Michuzi TV

NYUMBANI kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya. Nyumbani kwa Aliyekua Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Asha-Rose Migiro. Ndipo nyumbani pia kwa Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Prof Jumanne Maghembe.

Naizungumzia Wilaya ya Mwanga iliyopo Kilimanjaro. Wilaya ambayo licha ya kutawaliwa na milima mingi lakini ina miundombinu madhubuti ya barabara na nishati ya umeme pia.

Wilaya ya Mwanga licha ya kuwa na Tarafa sita lakini umaarufu wa Tarafa zake mbili za Ugweno na Usangi ndizo ambazo hasa zimeifanya wilaya hii kuwa maarufu na yenye kuvutia.

Siku chache nyuma nilikua wilayani hapo na nikapata wasaa wa kuzungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva ambaye alinieleza fursa mbalimbali zinazopatikana wilayani humo.

Lubuva anasema wawekezaji wanaweza kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri kutokana na ubora wa miundombinu iliyopo, mazingira mazuri ambayo kama Halmashauri wameyaweka kwa wafanyabiashara.

Amezitaja fursa kama Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na Utalii kama tu baadhi ya sekta ambazo mtu yeyote anayependa kuwekeza Mkoani Kilimanjaro na hasa Wilaya ya Mwanga anaweza kuwekeza na kutengeneza faida kubwa.

Akizungumzia sekta ya Ufugaji amesema kwa Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Mwanga ndio inayosifika kwa kuwa na wafugaji wengi huku ikiwa pia na mnada mkubwa wa Mgagao ambao umekua ukipokea wafugaji wengi wanaoleta mifugo yao hapo kwa ajili ya kuuza.

" Naweza kusema mnada huu wa Mgagao ni wa Kimataifa maana wilaya yetu imepakana na Nchi ya Kenya, hivyo pia tunapata hata wafugaji jamii ya Kimasai kutoka Kenya na hivyo kuongeza thamani ya mifugo yao," Amesema Lubuva.

Amesema kupitia mnada huo wananchi wa Mwanga wamekua wakipata kipato kizuri pindi wanapofanya biashara ya mifugo na kuongeza hali zao za kiuchumi.

Siyo tu kwenye mifugo, Wilaya ya Mwanga pia imebarikiwa kuwa na Bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo ni rasimali kubwa sana kwa serikali kwani Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lina mtambo mkubwa unaozalisha umeme.

Lubuva anasema uwepo wa bwawa hilo umekua fursa kwa wananchi kufanya biashara ya Uvuvi kwa kuvua samaki ambao wamekua wakiuzwa kwenye maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa jirani ya Manyara, Arusha na Tanga.

" Kwa mwekezaji wa biashara ya samaki kupitia bwawa hili anaweza kutengeneza fedha nyingi sana, ukiwekeza uvuvi kwenye bwawa hili una uhakika wa masoko kwenye mikoa minne na hata nje ya Tanzania kama ambavyo nimesema hapo awali kwamba wilaya yetu iko mpakani," Amesema Lubuva.

Kutokana na uwepo wa Bwawa la Nyumba ya Mungu na Ziwa Jipe tayari Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga chini ya Mkurugenzi Lubuva imeshatoa maelekezo ya kupima viwanja pembezoni mwa bwawa na Ziwa hilo ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza kwenye Hoteli za Kitalii na Michezo ya kwenye maji.

Amesema malengi ya halmashauri yake ni kuvutia wawekezaji zaidi kuja wilayani humo ili kuwekeza kwenye beach jambo ambalo pia litavutia watalii wengi kutembelea wilayani hiyo.

" Tunaamini kupitia mabwawa yetu haya kama na mipango iliyopo ya kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye Utalii kutaweza kuwavutia hata watalii wanaotembelea mbuga ya Mkomazi iliyopo wilayani jirani ya Same kuja kutembea kwenye beach zetu ambazo tutakua tumeziboresha vizuri," Lubuva.

Lubuva anasema eneo kubwa la Wilaya ya Mwanga lina misitu mingi hivyo tayari wameshatengeza mpango mkakati wao wa kuwatumia wataalam wao kuwekeza na kuamsha ari zaidi kwa wananchi kuwekez kwenye sekta ya nyuki.

Lakini pia amelizungumzia bwawa la Kisanjuli ambalo licha ya kuwepo wilayani hapo kwa miaka zaidi ya 50 limekua halitumiki kwa muda mrefu na tayari ameshawagiza wataalam wake kuandaa mpango mkakati wa kuhakikisha linaanza kutumika mapema kwa shughuli za uwekezaji ili kuiongezea halmashauri mapato na kuwa pia kivutio cha Wilaya hiyo.

Lubuva ambaye awali kabla ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mwanga alikua ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Osterbay jijini Dar es Salaam amewataka wenyeviti na watendaji wengine wenye nafasi za chini kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu ili kuweza kupanda juu zaidi.

' Nimshukuru sana Rais Dk John Magufuli kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa halmashauri. Alinipa fursa kubwa sana ambayo kwa hakika kitu pekee cha kumlipa ni kufanya kazi kwa bidii na kuwatumikia watanzania ambao walimuamini yeye na kumpa ridhaa ya kuwaongoza.

Hakuna nafasi ndogo mbele ya utendaji uliotukuka kwa wananchi wako. Niwatie shime wenyeviti wenzangu wa mtaa kufanya kazi kwa bidii na kwa uzalendo," Amesema Lubuva.
 Bwawa la Kisanjuli ambalo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva amesema litaanza kutumika katika Ufugaji wa Samaki baada ya kuagiza wataalam wake kuandaa mpango mkakati. Kwa mbele Misitu inayoonekana amesema itatumika kwa ajili ya Ufugaji wa Nyuki.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva akizungumzia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika halmashauri hiyo.
 

No comments: