MFANYAKAZI KAMPUNI YA GLOTEL LTD APANDISHWA KIZIMBANI KWA KESI YA UHUJUMU UCHUMI

MFANYAKAZI wa Kampuni ya Glotel Ltd, Jousia Msophe (32), Mkazi wa Kigamboni Kibugum jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya wizi wa kuaminiwa na kutakatisha kiasi cha Sh. Milioni 158.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Faraji Nguka amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,  Vicky Mwaikambo kuwa, kati ya Juni Mosi na Septemba 26 mwaka 2019 mshtakiwa aliiba sh. milioni 158 kutoka kwenye kampuni ya Glotel Ltd ambazo alikuwa amepewa na kuaminiwa kwa ajili ya biashara.

Imeendelea kudaiwa kuwa, mshtakiwa Jousia alijipatia kiasi hicho cha fedha huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na pia shtaka la utakatishaji fedha halina dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 4, mwaka huu.

No comments: