Mdau wa Maendeleo atoa vifaa kujikinga na corona Kondoa

Mmiliki wa mabasi ya Machame William Lucas ametoa sabuni na vitakasa mikono kwa ajili ya kuwasaidia watu waliokatika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya Corona katika Wilaya ya Kondoa na Chemba.

Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ilifanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wawakilishi wa vituo vya kulelea watoto yatima na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi hivi karibuni.

Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota amemshukuru mdau huyo na kumuahidi kuwa vifaa hivyo vitafikishwa kwa walengwa waliokusudiwa na si vinginevyo na kuwataka wadau wengine kuiga mfano wa mdau huyo.

“Bwana Lucas ameguswa sana jinsi Serikali inavyopambana na janga hili la Corona, na ameona ni vyema kushiriki katika mapambano hayo ambapo ametoa chupa 800 za sabuni ya maji pamoja na chupa 720 za vitakasa mikono, msaada huu utakwenda moja kwa moja kwa walengwa ambao ni vituo viwili vya kulelea watoto yatima, Polisi na Magereza pamoja na Vituo vyote vya Afya na Hospitali “.Alisisitiza Mhe. Makota.

Hata hivyo aliongeza kuwa pamoja na kutoa msaada huo katika ukaguzi wa mabasi uliofanya na Kmati ya Ulinzi na usalama mabasi ya kampuni ya Machame yapo mstari wa mbele kwa kuhakikisha taratibu zote za kupambana na maambukizi ya virusi ya Corona zinafuatwa na kuwasihi wamiliki wengine kuendelea kuchukua tahadhali zinazotolewa na wataalamu wa afya jinsi ya kujikinga na corona kwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kila mara.

Akiongea katika hafla hiyo Mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya Machame Bwana William Lucas amesema kuwa anategemea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wengine ili kwa pamoja waunganishe nguvu zao katika kuendelea kupambana na janga hilo la Corona ambalo limekuwa kikwazo kikubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kondoa Bwana Nicholaus Kasendamila amesema kuwa msaada huo ni msaada mkubwa na muhimu kwani umeisaidia Serikali kupambana kudhibiti hali ya Corona nchini na kumuomba bwana Lucas kuwa balozi wa kuhamasisha wengine kujitoa na kusisitiza kuendelea kuwa pamoja katika kukabiliana na janga hili kwa pamoja.

Hata hivyo mmoja wa wanufaika wa msaada huo ambaye ni mlezi msaidizi wa kituo cha Poloni Mission Sista Monica Irine amemshukuru mdau huo kwa upendo na moyo wa imani wa kuamini kuwasaidia wasiojiweza bila malipo yoyote na anaimani Mwenyezi Mungu atambariki kwa jambo hilo.

Mkuu wa Wilaya amepokea vifaa vya kujikinga na Corona kutoka kwa mdau huyo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa harakati za kupambana na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ambapo hafla hiyo ilihudhuliwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali, waandishi wa habari pamoja na wananchi.
 Bwana William Lucas mmiliki wa mabasi ya Machame (Kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Kondoa Mhe. Sezaria Makota vifaa kwa ajili ya kupambana na kuenea kwa virusi vya Corona.

 Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezaria Makota (kulia) akimkabidhi sabuni ya kunawia mikono mlezi msaidizi wa kituo cha kulelea watoto cha Poloni Mission Sista Monica Irine ikiwa ni sehemu ya msaada uliotolewa na mmiliki wa mabasi ya Machame
 Mkuu wa gereza la Kondoa  Mrakibu Julias Yona akipokea sabuni za kunawia mikono kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa na Mmiliki wa mabasi ya Machame  kwa ajili ya matumizi ya gereza la Kondoa.
OCD wa Kondoa Mohamed Kitia akipokea msaada wa sabuni kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kondoa na Mmiliki wa mabasi ya Kondoa kwa ajili ya matumizi ya Kituo cha Polisi Kondoa.

No comments: