KAMPUNI YA QWIHAYA YAUNGA MKONO SERIKALI VIFAA KINGA VYA CORONA STENDI YA MAFINGA

Na Matukiodaimablog.

Kipima joto kilichotolewa na Kampuni ya Qwihaya General Enterprises Co Ltd kimesababisha wananchi wanaofanya kazi stendi ya Mafinga wilayani Mufindi kusimamisha shughuli zao kwa muda ili wapime joto la miili yao.

Wananchi hao wakiwepo wapiga debe na wafanyabiashara ndogo ndogo walimteua mwenzao, akajifunza kukitumia na baadae walipanga foleni ili kila mmoja apime kujua joto la mwili wake.

Kifaa hicho, matenki mawili ya kuhifadhia maji na vitakasa mikono ni miongoni mwa misaada iliyotolewa na kampuni hiyo katika mwendelezo wa kampeni yake ya kupambana na maambukizi ya corona katika mji wa Mafinga,

Akikabidhi msaada huo, Meneja wa Kampuni ya Qwihaya, Ntibwa Mjema amesema stendi ni kati ya maeneo yenye mikusanyiko ambayo watu wanapaswa kuwa makini kwa kufuata taratibu za afya.

Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo, baadhi ya watu wanaofanya kazi stendi walishukuru kwa msaada huo kwa sababu hawakiwa na vifaa vya kujikinga.

"Hili tenki la maji likijaa tutatumia bila kujibana na hiki kipima joto kinaongeza hadhi ya eneo letu, ndio cha kwanza kuletwa," amesema mmoja wa wapiga debe, Frank Kalinga.

Kwa upande wake, Ramadhani aliiomba Serikali kudhibiti mlundikano wa watu kwenye magari ya vijijini kujilonda na ugonjwa huo.

Qwihaya ni kampuni inayomilikiwa na mzalendo Leonard Mahenda ikimiliki viwanda vya kutengeneza mbao mkoani Iringa na Kigoma.












No comments: