IBADA YA KWANZA MSIKITI MPYA WA BAKWATA YAFANYIKA, DK. BASHIRU AHUSISHWA

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu na wasio waumini jijini Mwanza wametakiwa kuendelea kuchangia na kukamilisha ujenzi wa Msikiti mpya wa Ijumaa wa Abubakar Zuberi Mbwana (Mutfi wa Tanzania), unaomilikiwa na Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa Mwanza.

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke alisema jana kuwa msikiti huo umeanza kutumiwa kwa ibada na waumini wa dini ya Kiislamu wakati huu wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku ufunguzi rasmi ukisubiri kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na kirusi cha Corona.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha waumini wa dini hiyo misikitini na kwenye jamii kujilinda na maambukizi y ugonjwa wa Corona (Covid-19) kuhakikisha wanavaa barakoa,wanatumia vyakula bora (milo iliyokamilika) na matunda yenye vitamini C ili kujiweka vizuri kiafya.

Alisema uamuzi wa kuanza kutumika kwa msikiti huo Mkuu wa Bakwata mkoani hapa kwa ibada umefanyika ili kuwaepusha baadhi ya waumini waliochangia sadaka zao kuujenga wasikose fadhila za mwezi Mtukufu wa Ramdhani licha kuwa haujakamilika bado na kuwaomba wenye uwezo waendelee kuchangia ili kukamilisha ujenzi huo.

“Leo tumeanza kuswali 13 ya Ijumaa ya Ramadhani katika Msikiti Mkuu wa Baraza hilo japo haujakamilika.Tumefanya hivi ili kuwafanya baadhi ya waumini waliotoa sadaka zao kwa ajili ya ujenzi ili wasikose fadhila za mwezi huu na tunashukuru Mwenyezi Mungu mahudhurio yalikuwa makubwa,”alisema Sheikhe Kabeke.

Aidha Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza Pia alimshukuru Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally kwa mchango wake wa saruji mifuko 100 akiwemo mfanyabiashara mmoja ambaye hakumtaja kwa michango hiyo iliyowezesha kufanyika kwa ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada.

“Mtu mwenye kutoa ama kujenga nyumba, hatoi kwa utashi wake bali anatoa kwa imani halisi ya dini yake, nitumie fursa hii kumshukuru Dk. Bashiru Ally (Katibu Mkuu wa CCM) aliyechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huu mwaka jana lakini pia wahisani wengine waliojitoa kuchangia hadi tulipofikia kuezeka na msikiti huu ni wa kihistoria,”alisema Sheikhe Kabeke.

Katika hotuba yake ya swala ya Ijumaa Sheikhe huyo wa mkoa, alielezea umuhimu wa kumi la 13 la Ramadhani, ambalo limegawanyika katika mafungu matatu, moja rehema, pili msamaha na la tatu ni kukombolewa na moto kwa kufanya ibada, kusaidia wajane na yatima pamoja na ubora wa mtu anayetoa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za ibada.

Alifafanua kuwa licha ya Bakwata kuwa na misikiti mingi haikuwa na msikiti wake mkuu badala iliteua msikiti mkuu wa kuendeshea ibada ya swala ya siku ya Ijumaa na si kwamba anawabeza waliotangulia la hasha na kutoa wito kwa wenye uwezo waendelee kuchangia waufanye ukamilike, uwe na hadhi yake. 

Aliwasitiza waumini wa dini ya kiislamu kuacha kubeza maelekezo ya kujikinga kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona (Covid-19) badala yake wazingatie iwe misikitini na kwenye jamii kujilinda na kuhakikisha wanavaa barakoa,wanakula milo iliyokamilika na matunda ya kujenga mwili. 

 Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke akiendesha Ibada ya swala ya Ijumaa ikiwa ni siku 13 ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ibada iliyofanyika juzi katika msikiti mpya wa Bakwata wa Abubakar Zuberi Mbwana, jijini Mwanza.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, alhaji Hasani Kabeke kuomba dua nje  ya misikiti mpya wa Bakwata wa Abubakar Zuberi Mbwana kabla ya kuanza kutumika kwa ibada ya Ijumaa ya 13 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani juzi (jana). PICHA NA BALTAZAR MASHAKA

No comments: