HUU NDIO MPANGO MKAKATI WA JESHI LA POLISI MBEYA KUELEKEA SIKUKUU
Katika kuelekea sikukuu ya Eid El fitr Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kikamilifu kusimamia usalama katika kipindi chote cha maadhimisho ya sikukuu ya EID EL FITR kwa kuhakikisha sherehe hizi zinafanyika kwa Amani na Utulivu.
Kwa kutambua kuwa Mkoa wetu unapakana na nchi jirani ya Malawi [Kasumulu] tumejipanga kuimarisha ulinzi na kuendelea kudhibiti uhalifu katika vipenyo vyote [njia zisizo rasmi]. Pia kuendelea na zoezi la kukagua watu wanaopita mpakani ili kujiridhisha kuhusu usalama wa Afya zao katika kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu @ Corona [COVID 19].
Kuelekea kipindi hiki cha sikukuu, waumini wa dini ya kiislamu ushiriki katika swala ya EID ambayo kwa mwaka huu itafanyika kwa kufuata taratibu zote za Afya, hii ni kwa ajili ya kuendelea kuchukua tahadhari ya kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu [COVID 19]. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa viongozi katika misikiti kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri hasa katika suala la ulinzi kwa kutumia kamati za ulinzi na usalama zilizopo ili kuhakikisha hali ya usalama katika maeneo ya ndani na nje ya misikiti.
Aidha tumejipanga vizuri katika kuhakikisha watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara wanafuata na kutii sheria za usalama barabarani katika maeneo yote. Pia katika kipindi hiki cha sikukuu tutaendelea na utaratibu wetu wa kupitisha magari kwa awamu katika maeneo yenye milima na miteremko mikali kama vile Mlima Nyoka, Iwambi, Mwansekwa, Igawilo na Kanyegele @ Uwanja wa Ndege. Aidha kutokana na janga la Corona, tumejipanga kuhakikisha vyombo vyote vya usafiri Daladala na Bajaji zinabeba abiria kulingana na siti zilizopo pamoja na kuhakikisha dereva na abiria wote wanafuata taratibu za Afya kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Corona kwa kuvaa barakoa.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe na maeneo ya fukwe kule Matema Wilayani Kyela.
Hakutakuwa na Disco Toto, hivyo tunawataka wazazi na walezi kuendelea kuwalinda watoto kwa kuwaepusha na mazingira yasiyo salama kwao.
Wito wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzingatia ulinzi wa watoto, na pia kuwaepusha watoto na matembezi au safari zisizo kuwa za lazima pamoja na mikusanyiko isiyo kuwa ya lazima ili kuwaepusha na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Homa Kali ya Mapafu [COVID 19]. Pia ili kuepuka watoto kupotea katika kipindi cha sikukuu, wazazi na walezi wanapaswa kuongeza umakini zaidi katika uangalizi wa watoto wao kila mahali watakapokwenda iwe ni makanisani au misikitini.
Pia tunasisitiza ulinzi na usalama katika makazi yetu, kuhakikisha kwa wale wanaotoka kwenda Msikitini kwa ajili ya swala ya EID au Kanisani kuhakikisha wanaacha waangalizi katika makazi pia kuhakikisha tunajilinda kwa kufunga milango na madirisha ili kuepuka uhalifu katika nyumba zetu.
Aidha nasisitiza utoaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu kupitia namba za simu zifuatazo:-
RPC…………………………………………………………….0715 009 931
OPERATION OFFICER……………………………………..0737 792 510
RCO…………………………………………………………….0658 376 052
RTO…………………………………………………………….0658 376 472
OCD MBEYA…………………………………………………0659 884 996
OCD MBALIZI………………………………………………..0655 248 381
OCD CHUNYA………………………………………………..0659 885 384
OCD MBARALI……………………………………………....0659 885 948
OCD RUNGWE……………………………………………….0659 885 253
OCD KYELA…………………………………………………..0659 887 919
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia DAMAS KALINGA [39] Mkazi wa Igohole, Wilaya ya Mufundi, Mkoa wa Iringa kwa tuhuma za mauaji ya Mjomba wake aitwaye LEMS MDEMU [42] Mkazi wa Mafinga baada ya kutokea ugomvi kati yao uliosababishwa na ulevi.
Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 21.05.2020 majira ya saa 18:00 jioni huko Soko la Vilabuni, Kijiji cha Mabadaga, Kata ya Mapogoro, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya ambapo mtuhumiwa alimsukuma marehemu na kudondokea jiwe sehemu ya kisogoni na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa matibabu. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu. Upelelezi unaendelea.
KUPATIKANA NA MALI IDHANIWAYO KUWA NI YA WIIZI.
Mnamo tarehe 21.05.2020 majira ya saa 09:30 asubuhi huko Kitongoji cha Machinjioni, Kata ya Makongolosi, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata AMOSI MAIKO [26] mkazi wa Makongolosi akiwa na Tv moja, Redio, Sub-woofer, nguo aina mbalimbali na vifaa vya pikipiki aina mbalimbali vidhaniwavyo kuwa ni ya wizi. Upelelezi unaendelea.
KUPATIKANA NA DAWA ZA BINADAMU BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 21.05.2020 majira ya saa 12:30 mchana huko Kitongoji cha Nazareth, Kata ya Serengeti, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walimkamata REHEMA JOHN [24] mkazi wa Kilambo akiwa na dawa za binadamu aina mbalimbali bila kuwa na kibali zikiwa ndani ya chumba anachoishi. Ufuatiliaji unaendelea.
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
No comments: